FIGO KATIKATI YA SHABANI RAMADHANI NA NSAJIGWA
Kikosi cha wakongwe wa Real Madrid kimewaonyesha soka wakongwe wa Tanzania kwa kuwachapa mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Kikwete.
Mabao ya Real Madrid, yote matatu yalifungwa na Ruben de la Red ambaye alianza kufunga moja katika kipindi cha kwanza.
Lakini Tanzania Eleven wakasawazisha bada ya Roberto Rojas kujifunga wakati akijaribu kuokoa.
Kipindi cha pili, De la Red akafunga mengine mawili, moja likiwa la mkwaju wa penalty.
Luis Figo ndiye alikuwa kivutio zaidi kwa mashabiki wengi waliojitokeza kwenye uwanja huo.
Mashabiki wengi walikuwa wakimshangilia wakati akiwahenyesha mabeki Shadrack Nsajigwa, Mecky Maxime na Salum Sued.
Madrid ndiyo walikuwa kivutio zaidi kutokana na kucheza kwa kuonana zaidi.
Pasi zao zilikuwa za uhakika kuliko kikosi hicho chini ya Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
DE LA RED AKIKABWA NA ATHUMANI CHINA NA HABIB KONDO
Hata hivyo, safu ya ushambuliaji ya Tanzania Eleven iliyoongozwa na Madaraka Selemani na Kali Ongala ilionekana kutokuwa na makali sana.
Ongala, Sabri Ramadhani ‘China’ na Athumani ‘China’ ndiyo walionyesha uhai zaidi katikati.
Lakini bado wasingeweza wenyewe hivyo kufanya kuwe na ugumu.
Mwisho, Rais Kikwete aliwakabidhi kombe Madrid ikiwa ni ishara ya kushinda mechi hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya TSN na kudhaminiwa na makampuni kadhaa kama Sapphire Court Hotel, Fast Jet, Bin Slum Tyres, Championi na TSN yenyewe.