Featured Posts

Sunday, August 31, 2014

HII KALI. WAZIRI MKUU PINDA AWAKIMBIA WAANDISHI WA HS

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda jana
alilazimika kutumia mlango wa uani
kuondokea badala ya ule mkuu kwa kile
kinachohisiwa kuwakwepa waandishi wa
habari waliokuwa wakifuatilia ufunguzi
wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya
nje na mazingira kutoka nchi za Afrika.
Pinda ambaye alikuwa akifungua
mkutano huo, aliondoka mara tu baada ya
kumaliza shughuli iliyompeleka huku
akiacha kushiriki tukio la kupiga picha
lililoandaliwa kwa ajili yake upande wa
lango kuu wa ukumbi huo ambako
waandishi walikuwa wakimsubiri kwa
ajili ya kufanya naye mahojiano.
Awali wakati Pinda akihutubia mkutano
huo uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi
wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam,
baadhi ya maofisa wa itifaki walionekana
wakisimamia zoezi la kupanga viti kwa
ajili ya tukio la picha ya pamoja ambalo
Waziri Mkuu huyo kama mgeni rasmi
ilitakiwa ashiriki.
Ni maofisa hao pamoja na baadhi ya
watumishi wa idara zinazohusika na
mkutano huo, ndio waliowaelekeza
baadhi ya waandishi wa habari ambao
hawakubahatika kuingia ndani kusubiri
katika eneo hilo la lango kuu ili waweze
kufanya mahojiano na Pinda hata hivyo
ahadi hiyo haikutimia.
Hatua hiyo ndiyo iliyoibua hisia kwamba
huenda, Pinda alifanya hivyo kukwepa
maswali ya waandishi wa habari hasa
kutokana na kuwepo kwa taarifa
zinazodai kuwa ametangaza dhamira yake
ya kuwania ukuu wa dola mwaka 2015.
Tangu taarifa hizo ziripotiwe kwa mara ya
kwanza na vyombo vya habari Jumapili
iliyopita, si Pinda wala wasaidizi wake wa
karibu ambao walijitokeza kuthibitisha
juu ya taarifa hizo.
Kutokana na hilo vyombo vya habari
nchini vimekuwa vikimtafuta Pinda ili
aweze kuzungumzia habari hizo, ambazo
anadaiwa kuzitoa mbele ya wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa kutoka mikoa ya Kanda ya
Ziwa aliokutana nao Ikulu ndogo ya jijini
Mwanza, Jumamosi iliyopita.
Katika tukio la jana wakati waandishi
wakimsubiri nje ya lango kuu, Pinda
alionekana akishuka chini na kuingia
katika eneo la pembeni ya ukumbi,
ambako inasemekana eneo hilo lina
mlango wa nyuma wa kutokea nje ya
ukumbi.
Waandishi hao, kwa matumaini
waliendelea kumsubiri Pinda kwa zaidi
ya dakika kumi bila mafanikio, huku viti
vilivyoandaliwa kwa ajili ya picha ya
pamoja vikiwa vimetelekezwa na
mkutano ukiendelea kama kawaida ndani
ya ukumbi huo.
Baada ya muda alijitokeza kijana ambaye
inasemekana ni mmoja wa wafanyakazi
kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira akisema kuwa; “Jamani
tuliwaalika watu wachache Waziri Mkuu
ameshamaliza na ameondoka, kama kuna
mtu hajamsikiliza Press release (taarifa ya
vyombo vya habari) ya Waziri Mkuu ipo
akatoe ‘photocopy’ karatasi ipo kwa yule
dada, (huku akionyesha mmoja kati ya
waandishi waliokuwa ndani ya ukumbi na
kwa wale wa Tv naomba mchukue kwa
kaka pale wa Tumaini.”
Akiwa mkoani Mwanza wiki iliyopita,
Pinda anadaiwa kuwaeleza wajumbe hao
wa CCM kuwa ameamua kuwania nafasi
ya Urais baada ya kushawishiwa na
viongozi wakuu wastaafu na viongozi wa
dini.

TUMEAMIA HUKU