Chande Abdallah na Deogratius Mongela
FUNDI ujenzi aliyefahamika kwa jina la Omari Mkulu (25) amedaiwa kuuawa na kutupwa ndani ya bwawa baada ya kudaiwa kutoweka nyumbani kwa takriban siku tatu.
FUNDI ujenzi aliyefahamika kwa jina la Omari Mkulu (25) amedaiwa kuuawa na kutupwa ndani ya bwawa baada ya kudaiwa kutoweka nyumbani kwa takriban siku tatu.
Tukio hilo lilitokea maeneo ya Mabwawa Saba, Mabibo jijini Dar ambapo majirani wa eneo hilo walidai kuwa waliiona maiti ya Omari ikiwa inaelea kwenye moja ya bwawa eneo hilo lakini kutokana na maiti hiyo kuvimba haikuwa ikitambulika.
Kwa mujibu wa marafiki zake ambao walifanya jitihada za kusafiri hadi Chanika kwa baba wa marehemu ili kuhakikisha kama kweli maiti ile ilikuwa ni ya Omari na kuthibitisha kuwa ni kweli, walidai kuwa kabla marehemu hajatoweka, alilipwa fedha zake za ujenzi ambapo ilidaiwa kuwa alikwenda kuzitumia kwenye pombe mpaka usiku wa manane.
“Siku ile marehemu alikuwa amelewa sana kwa sababu alikuwa amepata fedha zake za malipo, tangu siku ile hakuonekana tena mpaka leo hii. Kwa kuwa sura na mwili wake umevimba tumezitambua nguo zake alizovaa,” alisema mmoja wa marafiki hao aliyeiomba hifadhi ya jina.
Waandishi wetu walipofika katika eneo la tukio, waliishuhudia maiti hiyo ikitolewa kwenye bwawa hilo ambapo umati wa watu waliofika katika eneo hilo walipewa nafasi ya kumtambua ambapo mmoja wa watu waliofika alidai kuwa mtu huyo ni jirani yake, akawaelekeza waandishi nyumbani kwa marehemu.
Waandishi wetu walifika nyumbani kwa marehemu na kuzungumza na mama mkubwa wa Omari aliyejitambulisha kwa jina la Zainabu Omari ambaye alisimulia kwa uchungu kuwa mwanaye huyo alitoweka nyumbani Agosti 10, mwaka huu baada ya kumpatia shilingi 2,000 alizomuomba.
“Siku hiyo alikuwa na shilingi 5,000 mimi akanipa shilingi 2,000 halafu akaniambia kuwa jioni ya siku hiyo kuwa akipata hela ataelekea kwa baba yake Chanika, sasa tulishangaa tu kikapita kimya hakurudi nyumbani kuaga wala kuchukua nguo zake mpaka sasa tumesikia amekutwa amefariki dunia bwawani,” alisema kwa uchungu mama huyo