Kwa muda mrefu wafuasi wa mwanamuziki Ally Salehe Kiba maarufu Alikiba, wamekuwa wakijiuliza sababu zilizomfanya mwimbaji huyo kukaa kando ya muziki kwa muda mrefu.
Alikiba ambaye aliachia wimbo wake wa mwisho “My Everything” Novemba 2012 hajawahi kuachia tena wimbo mwingine, licha ya kutoa kazi kadhaa alizokuwa akishirikishwa na mdogo wake msanii Abdu Kiba ukiwamo “Kidela”.
Starehe ilikaa kitako na msanii huyu aliyewahi kutamba na wimbo wake wa kwanza “Sinderela” mwaka 2007, nyumbani kwake Kunduchi Beach na ambapo aliainisha mambo makubwa matatu yaliyomfanya asimame kwa muda kuachia kazi za muziki.
“Kuna mambo matatu ya msingi niliyokuwa nayafanya kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Awali ya yote niliamua kusimama ili kumlea mwanangu, malezi ya mtoto yalinifanya niegemee huko hadi umri wake usogee ndipo nirudi kwenye muziki,” anasema pasipo kufafanua vizuri iwapo ni wa kike au wa kiume.
Anasema familia yake ni kitu chenye uthamani mkubwa kwake ndiyo maana alijitoa ili kuhakikisha inakaa sawa.
“Jambo la pili ambalo najivunia kulifanikisha kwa kipindi hiki, ni kuweza kumsimamisha sehemu nzuri mdogo wangu Abdu Kiba katika ramani ya muziki. Hili lilikuwa suala kubwa na nyeti kwangu kuhakikisha anatimiza ndoto zake nilijitahidi kumpa nyenzo ili na yeye ajulikane kwani nilimuona ana kipaji kikubwa,” anasema.
Jambo la tatu analifafanua kuwa ilimchukua muda kufikiria namna atakavyowaacha wasanii wengine Tanzania, na wao wajulikane ndani na nje ya nchi.
“Tatu niliona nitulize kichwa kidogo kwa kufanya biashara na pia kuwaacha wasanii wengine na wao kipaji chao kionekane na kuwapa nafasi ya kufanya vizuri ndani na nje ya nchi, nashukuru hilo limefanikiwa tena kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa kwa kipindi hicho wameibuka wengi ambao wameweza kufanya vizuri na kwa wale ambao walikuwepo kitambo wamepanuka zaidi kifikra,” anasema Alikiba.
Anasema kwa kipindi cha miaka mitatu aliyopumzika, amejifunza mengi na pia ameona kumekuwa na mapungufu katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya na maendeleo pia.
“Mapungufu yamekuwepo, lakini kuna mafanikio mengi pia, kuna baadhi ya wasanii wamefanikiwa kufanya muziki mzuri na kuutangaza kimataifa na wengine wametengeneza kazi nzuri, lakini kinachonitisha ladha ya muziki wetu asili hasa ya bongofleva, imepotea tumeanza kutengeneza muziki wenye utofauti mkubwa sana na kipindi cha nyuma, kwa kuiga ala ya muziki wa Nigeria na mataifa mengine,” anasema Alikiba.
Albamu mbili, singo mpya wiki ijayo
Alikiba aliyetamba na wimbo “Dushelele” miaka miwili iliyopita, ameweka wazi ujio wake wiki ijayo akiwa chini ya kampuni kubwa barani Afrika ambayo hajataka kuiweka wazi, anasema alikuwa ‘chimbo’ kwa takribani miaka miwili akiandaa kazi mpya ambapo amefanikiwa kukamilisha albamu mbili na punde kuachia singo mpya.