Featured Posts

Saturday, April 12, 2014

MAONI YA WAJUMBE ' WALIO WACHACHE' KATIKA KAMATI NAMBA NNE ILIYOWASILISHWA NA MHE. TUNDU LISSU!

Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote
imejengwa juu yao . Wakati Sura ya Kwanza
inagusa suala la muundo wa Muungano katika
ibara moja tu kati ya ibara tisa , Sura yote ya
Sita inahusu ‘ Muundo wa Jamhuri ya
Muungano. ’ Suala la Muungano na hasa
Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa
na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka
thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa
siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha
Mapinduzi (‘CCM’) , Idara ya Siasa na Uhusiano
wa Kimataifa ya chama hicho imetamka
kwamba “ muundo wa Muungano ndiyo moyo
wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine
zikae vipi . ”
Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba
Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita .
Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba
wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais
wa Zanzibar tarehe 30 Disemba , 2013 : “ Moja
ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa
hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa . . .
ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa
limekuwa juu ya muundo wa Muungano . ”[ 1]
Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na
uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge
Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake
Namba Moja hadi Kumi na Mbili zianze
kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu.
Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa
Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Mjadala wa Kamati Namba Nne kuhusu Sura
za Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia
umuhimu wa suala la muundo wa Muungano
katika mjadala mzima wa Rasimu . Kama
Taarifa ya Kamati yetu inavyoonyesha , Kamati
Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi
kuhusu suala hili katika ibara za 1 na 60 za
Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza,
wajumbe walio wengi walipata kura 22,
ambayo ndiyo theluthi mbili ya kura za
wajumbe wote 33 wa Tanzania Bara wa Kamati
Namba Nne . Kwa upande wa Zanzibar ,
wajumbe walio wengi walipata kura 9 ambayo
ni pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili
kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe
wote 19 wa Zanzibar.
Kwa upande wa ibara ya 60 , wajumbe walio
wengi walipata kura 22 za wajumbe kutoka
Tanzania Bara , ambazo ni theluthi mbili ya
idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania
Bara . Aidha , kwa Zanzibar, wajumbe walio
wengi walipata kura 8 , ambazo pia ni pungufu
ya kura 13 zinazotakiwa kufikisha idadi ya
theluthi mbili ya wajumbe wote 19 kutoka
Zanzibar. Kwa sababu hiyo , ibara za 1 na 60
za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na
Kamati Namba Nne kama inavyotakiwa na
kifungu cha 26 (2) cha Sheria na kanuni ya
64(1 ) ya Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Sasa tunaomba kwa ridhaa yako , tuwasilishe
hoja na sababu za maoni ya wajumbe walio
wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu
Sura hizi mbili ambazo ndio ‘ moyo wa
Rasimu. ’
SURA YA KWANZA
Sura ya Kwanza ya Rasimu inahusu ‘ Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania . ’ Sehemu ya
Kwanza ya Sura hiyo inazungumzia ‘ jina ,
mipaka , alama , lugha na tunu za Taifa. ’ Ibara
ya 1 inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania; ibara ya 2 inatangaza ‘ eneo la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’; na ibara
ya 3 inaweka utaratibu wa ‘ alama na sikukuu
za Taifa. ’ Vile vile ibara ya 4 inaweka utaratibu
wa lugha ya Taifa na lugha za alama , wakati
ibara ya 5 inahusu ‘ tunu za Taifa. ’
Kwa upande wake , Sehemu ya Pili ya Sura ya
Kwanza inaweka masharti ya ‘ mamlaka ya
wananchi , utii na hifadhi ya Katiba . Ibara ya 6
ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘ mamlaka
ya wananchi ’; ibara ya 7 inafafanua uhusiano
kati ya ‘ watu na Serikali’; ibara ya 8
inashurutisha ‘ ukuu na utii wa Katiba ’; na
ibara ya 9 na ya mwisho inaweka ‘ hifadhi ya
utawala wa Katiba. ’
IBARA YA 1
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Kama maelezo yake ya pembeni (marginal
note) yanavyoonyesha, ibara ya 1
inaitambulisha ‘ Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. ’ Ibara ya 1( 1) inatamka kwamba
“ Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo
imetokana na Muungano wa nchi mbili za
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964
zilikuwa nchi huru. ”
Kwa upande wake , ibara ya 1( 2) inafafanua
kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
“ ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata
mfumo wa vyama vingi vya siasa , usawa wa
binadamu, kujitegemea , utawala wa sheria ,
kuheshimu haki za binadamu na
lisilofungamana na dini. ” Mwisho, ibara ya 1 (3)
inatukumbusha kwamba “ Hati ya Makubaliano
ya Muungano . . . ndio msingi mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba
hii , kwa kadri itakavyorekebishwa , itakuwa ni
mwendelezo wa Makubaliano hayo . ”
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba
Nne wanapendekeza mabadiliko ya jina la nchi
yetu kutoka jina la sasa la ‘ Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ’ kuwa jina jipya la
‘ Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar. ’ Aidha , wajumbe hao
wanapendekeza kuacha kutajwa kwa Hati ya
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964
katika ibara ya 1( 1) na ( 3) ya Rasimu . Badala
yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo
iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za
Tanganyika na Zanzibar.
Kwa mapendekezo haya, ibara ya 1 (1)
itasomeka kama ifuatavyo: “ Shirikisho la
Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni
Shirikisho ambalo limetokana na Muungano
wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. ” Kwa mantiki
hiyo , ibara ya 1( 2) itasomeka: “ Shirikisho la
Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni
Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo
wa vyama vingi vya siasa , usawa wa
binadamu, kujitegemea , utawala wa sheria ,
kuheshimu haki za binadamu na
lisilofungamana na dini. ” Aidha , ibara ya 1(3 )
itasomeka: “ Katiba hii ndio msingi mkuu wa
Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar. ” Zifuatazo ni hoja na sababu za
mapendekezo haya.
SHIRIKISHO AU MUUNGANO ?
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Katika nusu karne ya uhai wake , nchi yetu
imeitwa ‘ Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ’
Hata hivyo , katika kipindi chote hicho, Katiba
na Sheria za nchi yetu hazijawahi kufafanua
kwa uwazi aina au haiba ya ‘ Muungano ’ huu .
Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu ni
kwamba katika nusu karne hiyo , kumekuwa na
mjadala mkubwa wa kikatiba, kisiasa na
kitaaluma kuhusu suala la kama Jamhuri ya
Muungano ni dola ya muungano (a unitary
state ), au ni dola ya shirikisho ( a federal
state ). Majibu ya swali hili yamekuwa na
athari za moja kwa utambulisho , haki , maslahi
na wajibu wa Washirika wa Muungano huo ,
yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa kwa
wananchi wa nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Kukosekana kwa ufafanuzi wa aina ya
muungano wetu haujawa suala la mijadala ya
kisiasa na kikatiba peke yake, bali kumekuwa
ni chanzo cha migogoro mikubwa ya kisiasa
baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii
ilianza tangu mwanzo kabisa wa Muungano
wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa
iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa
Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani
Mashariki kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, kati ya mwaka 1964 -1967 ulizuka
mgogoro mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa
Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu
ya Tanzania; kuunganishwa kwa vyama vya
ASP na TANU na kuundwa kwa CCM mwaka
1977, na katika mjadala wa marekebisho ya
Katiba wa mwaka na baadae ‘ kuchafuka kwa
hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar ’ mwaka
1983/1984 .
Baadae mwaka 1988 ulitokea mgogoro
mkubwa uliopelekea kung’ olewa madarakani
kwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad na baadae
kufukuzwa katika CCM; wakati wa harakati za
kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano
mwaka 1989 /1990 ; wakati wa mjadala wa
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya
siasa mwaka 1991 ; wakati wa sakata la
Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za
Kiislamu ( Organization of Islamic Countries -
OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala wa G - 55
na madai ya kuanzishwa kwa Serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994 ,
na Uchaguzi Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.
Milenia Mpya ilipoanza ilianza na mgogoro
kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2000 uliopelekea mauaji ya Januari 2001 huko
Zanzibar. Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro
juu ya suala la ugunduzi wa mafuta visiwani
Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa
Shirikisho la Afrika Mashariki na hivi karibuni
kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya
Katiba ya Zanzibar ya 1984 mwaka 2010 .
Zaidi ya migogoro hii , Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar
zimeunda tume na kamati nyingi ili kupata
dawa ya ‘ Kero za Muungano. ’ Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar peke yake imeunda tume
na kamati 13 katika kipindi kifupi cha miaka
12 kuanzia mwaka 1992 hadi 2004 ; wakati
Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda
tume na kamati nane kushughulikia matatizo
hayo . Licha ya jitihada zote hizo , ‘ Kero za
Muungano’ hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu .
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Tangu miaka ya mwanzo ya Jamhuri ya
Muungano kulikuwa na mitazamo miwili tofauti
miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa
Jamhuri ya Muungano . Mitazamo hii tofauti
inathibitishwa na kauli ya Mwalimu Julius K .
Nyerere, mwasisi na Rais wa Kwanza wa
Jamhuri ya Muungano katika Mkutano Maalum
wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika
Dodoma kati ya tarehe 24- 30 Januari, 1984 :
“ . . . Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa
jicho la Zanzibar ni wa shirikisho lakini
ukiangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni
Serikali moja. ”[2 ]
Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais
wa Zanzibar wakati huo , Alhaj Aboud Jumbe
Mwinyi aliyesema kwamba Muungano wa
Tanzania umeunda Shirikisho (Federation) na
sio Serikali moja ( Unitary State ) . Mjadala huo
ulipelekea ‘ kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar’ na kung’ olewa madarakani
kwa Jumbe, Waziri Kiongozi wake Ramadhani
Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw
Swanzy. Aidha, Wolfgang Dourado , aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya
Muungano inasainiwa, na mkosoaji mkubwa
wa Muungano huo , aliwekwa kizuizini kwa
kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe .
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Miaka kumi baada ya ‘ kuchafuka kwa hali ya
hewa ya kisiasa Zanzibar’ Jamhuri ya
Muungano ilikabiliwa na mgogoro mwingine
tena wa kikatiba na kisiasa , mara hii ukitokana
na Zanzibar kujiunga na OIC . Kitendo hicho
kilizua tafrani kubwa ya kisiasa pale Bunge la
Jamhuri ya Muungano lilipopitisha Azimio la
kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika
ndani ya Muungano mwezi Agosti , 1993 .
Azimio hilo liliungwa mkono na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano , kitendo kilichomfanya
Mwalimu Nyerere kuingilia kati na kuzima
jaribio hilo.
Baadae Mwalimu aliandika kitabu alichokiita
Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania
kilichochapishwa mwaka 1994 . Katika kitabu
chake, Mwalimu anarejea mkanganyiko ambao
umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu
kwa maneno yafuatayo:
“ Nchi zinapoungana na kuwa nchi moja
mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni
miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta
serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa
itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja .
Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua
madaraka fulani ambayo yatashikwa na
serikali ya shirikisho , na itakuwa na serikali
ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo
yaliyobaki . Mambo yatakayoshikwa na serikali
ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika
mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli
nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi
moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye
ushirikiano mkubwa katika mambo fulani
fulani . . . . Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa
ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya
shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili
za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya
moja. ”[ 3]
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Mwaka ambao Mwalimu Nyerere alichapisha
Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ,
Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na
Makamu Rais wake hadi Januari 1984 , Alhaj
Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya
wa Zanzibar wakati Muungano unazaliwa na
baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye
alichapisha The Partnership: Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya
Dhoruba . [ 4] Katika kitabu hicho, Alhaj Jumbe
anathibitisha kwamba “ Ibara za Mkataba wa
Muungano ziliweka bayana mfumo ambao
serikali kuu na serikali shiriki katika Muungano
kuwa na nguvu zinazoendeana , yaani , mfumo
wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa
mahakama , baraza la kutunga sheria na urais
baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi ,
na kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya
mamlaka yake. ”[ 5]
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Aina ya dola iliyotokana na Hati ya
Makubaliano ya Muungano haikuwahangaisha
waasisi wa Muungano ama viongozi wake
wakuu peke yao . Hata ndani ya makorido ya
mamlaka , mjadala juu ya suala hili umekuwa
mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali
mbali za kulichunguza . Kwa mfano, hata kabla
ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima
ya Tanzania na The Partner -ship , tarehe 6
Aprili , 1992 , Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk . Salmin
Amour aliunda Kamati ya Baraza la Mapinduzi
ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano
wa Tanzania, maarufu kama Kamati ya Amina
Salum Ali kutokana na jina la Mwenyekiti
wake. Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna,
ambaye ni mjumbe wa Bunge hili Maalum ,
alikuwa Katibu wa Kamati hiyo .
Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Amina
Salum Ali ililichunguza suala la aina ya
Muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano
ya Muungano . Jibu la Kamati hiyo lilikubaliana
na nusu ya hoja ya Mwalimu Nyerere na nusu
ya hoja ya Alhaj Aboud Jumbe: “ . . . Muungano
wa Tanzania, haidhuru unaitwa ‘ Union ’ , lakini
uko kati na kati baina ya ‘ Union’ na
Shirikisho . Kuwepo kwa Serikali ya Muungano
yenye madaraka makubwa ni kielelezo cha
sura ya ‘ Union’ . Sura hii inazidi kutiliwa nguvu
na kile kitendo cha Tanganyika kuvua
madaraka yake yote na kuyaingiza katika
Serikali ya Muungano . Kwa upande mwengine
kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
yenye madaraka kamili Zanzibar juu ya
mambo yote yasiyokuwa ya Muungano , ni
kielelezo dhahiri cha sura ya Shirikisho . Kwa
hivyo , Muungano huu ni wa aina yake. ”[ 6]
MTAZAMO WA KITAALUMA
Mheshimiwa Mwenyekiti ,
Hati ya Makubaliano ya Muungano wa Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar imejadiliwa sana na kwa miaka mingi
katika ulingo wa kitaaluma . Mjadala huu
umehusu, kwa kiasi kikubwa , aina na muundo
wa Muungano huu . Katika kitabu chake
Tanzania: The Legal Foundations of the Union,
kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwezi
Januari, 1990 , Profesa Issa Shivji alisema,
baada ya uchambuzi wa kina wa Hati ya
Muungano, kwamba Makubaliano ya
Muungano yalitengeneza katiba ya shirikisho .
Kwa mujibu wa Profesa Shivji, katiba za
shirikisho zina sifa kuu zifuatazo ambazo
alisema zipo katika Hati ya Muungano : [ 7]
a . Kuna mgawanyo wa wazi wa madaraka
kati ya serikali kuu na serikali za sehemu za
muungano ambayo yapo katika ngazi moja;
b. Mamlaka ya serikali kuu yaliyowekewa
mipaka ya wazi wakati mamlaka yaliyobaki
yako mikononi mwa serikali za sehemu za
muungano ;
c . Serikali zote , yaani serikali kuu na serikali
za sehemu za muungano zinagusa maisha ya
wananchi wao moja kwa moja tofauti na
serikali ya mkataba ( confederation) ambako
serikali za sehemu ndizo zinazogusa maisha
ya wananchi moja kwa moja. [ 8]
Kwa maneno ya Profesa Shivji, kwa
kuyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka
upande wa Zanzibar na Tanganyika na kwa
ujumla wao, “ . . . msingi wa shirikisho ndio
wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano
yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi kama katiba
ya shirikisho . ”[9 ] Kwingineko katika kitabu
hicho, Profesa Shivji alidai kwamba: “ Kwa
vyovyote vile , ni wazi kwamba Makubaliano ya
Muungano sio katiba ya muungano (unitary
constitution ). ”[ 10 ]

TUMEAMIA HUKU