Featured Posts

Friday, May 16, 2014

KABURI LA SHEHE YAHYA LABOMOREWA NA NDUGU, NINI KISA NA MKASA? MCHAPO WOTE HUKO HAPA

AKUBWA! Kaburi la aliyekuwa Mnajimu Mashuhuri Afrika Mashariki, marehemu Shehe Yahya Hussein limejengwa tena baada ya hivi karibuni kubomolewa na watu wasiojulikana, lakini sasa limedaiwa kujengwa Kikristo na chini ya kiwango!

Kaburi la aliyekuwa Mnajimu Mashuhuri Afrika Mashariki, marehemu Shehe Yahya Hussein baada ya kujengwa tena.
Akizungumza na Risasi Jumamosi juzi jijini Dar, msemaji wa familia ya Shehe Yahya, Maalim Hassan Yahya Hussein alisema kaburi hilo lipo kwenye Makaburi ya Tambaza karibu na Hospitali ya Muhimbili, Dar sanjari na lile la marehemu Shehe Kasim Bin Jumaa.
Alisema makaburi yote yalibomolewa wakati wa Operesheni Safisha Jiji ambapo serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alikataa jiji kuhusika.
Hata Maalim Hassan alikiri si serikali iliyoyabomoa makaburi hayo bali ni wahuni wachache, lakini akasema mkuu wa mkoa aliahidi kwamba serikali itayajenga upya tena kwa kuyaboresha.
Familia hiyo ikasema inashangazwa makaburi hayo kujengwa katika mfumo wa makaburi ya Kikristo jambo ambalo halitoi picha nzuri kwa sababu wako watu wanatoka nje ya nchi kuja Tanzania kutaka kuliona kaburi la Shehe Yahya.
FAMILIA KUBOMOA
“Makaburi yale yalitakiwa kujengwa kwa kutumia kokoto maalum ziitwazo ‘mable’ na kulikuwa hakuna sababu ya kujenga ngazi ambazo watu wanaweza kukaa kama kaburi la marehemu Steven Kanumba.
“Kama marehemu alipokuwa hai hakukaliwa kwa nini akiwa amekufa akakaliwe akiwa ndani ya kaburi? Kule ni kumkosea heshima.
“Sisi kama familia tumeamua kwamba, lazima tuyabomoe makaburi yote, la baba na lile la marehemu Shehe Kassim siku ya Jumamosi (leo) na kuyajenga upya tutakavyo sisi tena kwa gharama zetu, serikali  ibomoe matofali yao,” alisema Maalim Hassan.
Marehemu Sheikh Yahya Hussein enzi za uhai wake.
SHILINGI MILIONI 4.5 ZATAJWA
Akifafanua zaidi, Maalim Hassan alisema Manispaa ya Ilala jijini Dar ilitoa shilingi milioni 4.5 kwa kila kaburi kama gharama za ujenzi kwa kupitia ile ahadi ya mkuu wa mkoa baada ya kubomolewa usiku wa Aprili 12, mwaka huu lakini thamani ya ujenzi uliofanywa haufikii fedha hizo.
Aliendelea kudai kwamba anaamini kuna ufisadi mkubwa uliofanyika kwenye ishu hiyo na kwamba kitendo hicho ni sawa na kuwadhulumu marehemu hao.
Alipoulizwa ni nani aliyekabidhiwa jukumu la kusimamia ujenzi wa makaburi hayo, Maalim Hassan alimtaja Shehe Mohamed Mtulya ambaye ni kiongozi kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam.
Naye mtoto wa Shehe Kassim Jumaa, Mahmud Kassim alipozungumza na Risasi Jumamosi kuhusu hali ya makaburi hayo alisema na yeye hakubaliani na ujenzi huo akisisitiza kuwa yamejengwa tofauti na makubaliano na yanaonesha tofauti na ya Kiislamu kwa sababu yana sura ya Kikristo.
“Hata mimi sikubaliani na jinsi makaburi yale yalivyojengwa. Kwanza yana sura ya Kikristo. Hatukukubaliana hivi,” alisema.
USHUHUDA WA MTU BAKI
Naye mkazi mmoja wa jijini Dar ambaye alikutwa na waandishi wetu eneo la makaburini, alisema ni kweli ujenzi wa makaburi hayo ni sawa na ule wa Kikristo kwa vile hata sehemu ya wazi iliyoachwa juu ni ndogo sana wakati kaburi la Kiislamu linatakiwa sehemu yote ya juu kuwa wazi na kuwa la chini.
“Shehe Yahya alikuwa mtu mkubwa sana. Kama mnakumbuka alikuwa akiongoza kwa kukariri  Aya za Kuran Afrika Mashariki, kaburi lake lilitakiwa kuwa linalotambulisha Uislamu wake safi,” alisema mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ally Maulidi.

SHEHE MOHAMED MTULYA ANASEMAJE?
Gazeti hili lilimtafuta Shehe Mohamed ambaye anatajwa kuhusika na jukumu la kusimamia ujenzi wa makaburi hayo. Alipopatikana alisema hakuna kaburi la Kiislamu linaloweza kujengwa kwa shilingi milioni 4.5 bila kufafanua maana ya kauli yake hiyo.
Alipoulizwa gharama alizotumia kujenga makaburi hayo, alisema:
“Unajua mimi si msemaji wa serikali, andika unavyoona na mimi nitajibu.”
Msemaji wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck  Sadik hawakupatikana kwenye simu zao licha ya kupigiwa mara kadhaa.
TUREJEE NYUMA
Shehe Yahya alifariki dunia Mei 20, 2011 jijini Dar es Salaam na kuzikwa Mei 21 kwenye makaburi hayo.
Shehe Kassm alifariki dunia mwaka 1994 na kuzikwa papohapo, wote walikuwa marafiki wakubwa

TUMEAMIA HUKU