Lile sekeseke la viungo vya binadamu kukutwa kwenye dampo jijini Dar
es Salaam limechukua sura mpya huku mambo mazito 10 yakiibuliwa na
gazeti makini na lenye heshima kubwa, Amani.
Tukio hilo lilivuta hisia za wakazi wa Bunju na maeneo mengine ya Jiji la Dar na viunga vyake hivyo kusababisha minong’ono mingi huku baadhi yao wakihusisha tukio hilo na imani za kishirikina!
Kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kiliingia kazini tangu usiku wa tukio na kufanikiwa kugundua mazito hayo ambayo hayapatikani mahali popote zaidi ya kwenye gazeti hili.
WAHUSIKA
Habari za uhakika zinasema kuwa, viungo vya miili hiyo vilidaiwa kutoka katika Hospitali ya IMTU iliyopo Mbezi–Beach jijini Dar es Salaam ambayo ndani yake ina chuo cha utabibu.
Ilidaiwa kwamba, viungo hivyo vilikuwa miili kamili ambayo hutumika kwa ajili ya mazoezi ya udaktari kwenye vyumba vya upasuaji.
“Ni kawaida, vyuo vyote vinavyohusiana na udaktari huwa wanakuwa na maiti ambazo huzifanyia experiment (majaribio au mazoezi) ya surgery (upasuaji). Lakini pamoja na hivyo, huwa haitakiwi kuonekana baada ya kumaliza matumizi hayo,” anaeleza mmoja wa madaktari bingwa wa hospitali moja kubwa jijini Dar kwa sharti la kutotajwa gazetini.
Suala la Hospitali ya IMTU kuwa wahusika wa viungo hivyo halina ubishi, kwani hata Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova, juzi alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alithibitisha hilo.
IDADI YA MAITI
Akifafanua zaidi, Kamanda Kova alisema mpaka sasa haijajulikana viungo hivyo vilikuwa ni maiti za watu wangapi lakini uchunguzi bado unaendelea.
Alisema, jeshi lake lilikamata mifuko 85 iliyokuwa na viungo hivyo ikiwa ni vichwa, miguu, mikono, mapafu na mifupa ya sehemu mbalimbali za mwili wa binadamu.
VIUNGO VINGI VYA WANAWAKE
Uchunguzi umeonesha kwamba katika viungo hivyo ingawa havikuungana, sehemu kubwa ni vya wanawake. Hilo lilithibitika baada ya kuonekana kwa vipande vingi vya matiti ya wanawake.
KWA NINI VILIKUWA VIMEKAUKA?
Kwa mujibu wa daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (jina lipo), miili inayotumika kufanyiwa mazoezi na wanafunzi wa vyuo vya tiba hukaushwa ili isioze (cadevier). Lengo ni kuifanya idumu kwa muda mrefu ili wanafunzi mbalimbali waweze kufanyia mazoezi.
Habari za ndani zilizonaswa na Amani zinasema kuwa, daktari mmoja wa hospitali hiyo (jina tunalo) alipewa jukumu la kupeleka miili (siyo viungo) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili ikachomwe kwa sababu tanuri la kuchomea kwenye hospitali hiyo liliharibika.
Inadaiwa pale Muhimbili aliambiwa atoe Sh. milioni nne, akarudi kazini kwake na kuweka mezani madai hayo ambapo uongozi ulimkabidhi kiasi hicho cha fedha.
“Yule daktari akatoka na miili kwenye lori, lakini badala ya kuipeleka Muhimbili, yeye aliwapa watu kaisi cha fedha ili wakaitupe dampo na kiasi kingine akatia ndani.
“Uongozi ulijua miili imekwenda kuchomwa Muhimbili mpaka habari za kuonekana kwa viungo dampo zilipoibuka wakashangaa. Lakini wanajiuliza wao walitoa miili mbona vimekutwa viungo? Jamaa naye katimka, hajulikani alipo,” kilisema chanzo kimoja hospitalini hapo.
MAITI ZINAPATIKANAJE?
OFM ilifanikiwa kugundua kwamba, miili ya kufanyia mazoezi kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya tiba hupatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo si kosa la jinai. Kuna madai huuzwa kwa bei mbaya ambayo haikutajwa.
“Vyuo vyote vya utabibu kwa hapa Dar huchukua maiti kwetu. Ni Muhimbili pekee ndiyo wenye kibali cha kutoa maiti. Ni jambo la kawaida kabisa, tatizo ni kuonekana huko mitaani ikienda kutupwa, ule si utu na hata taaluma inakataa,” alisema mmoja wa madaktari wa Muhimbili akifafanua suala hilo.
SABABU ZA MIILI KUTOLEWA
Akifafanua zaidi, daktari huyo alisema: “Hata hivyo lazima niweke sawa, maiti zinazotolewa ni zile ambazo zimekaa hapa hospitalini kwa miezi mitatu (siku 90) bila kupata ndugu. Hospitali ikijiridhisha kuwa maiti haina mwenyewe basi huweza kutolewa.”
KWA NINI BUNJU?
Habari kutoka vyanzo mbalimbali vya OFM, zinaeleza kwamba tatizo si hospitali kumiliki viungo vile, bali ni kuonekana hadharani tena vikiwa vimerundikwa kama havikuwahi kuwa na nafsi.
“Lile gari lilikuwa linakwenda kutupa porini, which is not right (jambo ambalo siyo sahihi). Baada ya wanafunzi kumaliza mazoezi, miili hutakiwa kuteketezwa kwa dawa maalum iitwayo incinerator.
Mwananchi mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa Chuo cha IMTU aliandika kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa iliwahi kutokea miaka ya nyuma scenario (suala) kama hiyo ambapo mwanafunzi (hakutaja chuo) aliyeonekana na mkono (wa binadamu) mtaani of which (kitu ambacho) hairuhusiwi hata kutoka na gloves (glovu) nje ya chumba. Ishu ile ilileta mtafaruku mkubwa.
STORI YENYEWE
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, uchunguzi wa awali umebaini kuwa viungo vile vilitolewa IMTU na mpaka sasa wameshawakamata watu nane wakiwemo madaktari kwa upelelezi zaidi.
WIMBI LA WATU KUPOTEA DAR
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Amani walionesha wasiwasi kuhusu kupatikana kwa viungo hivyo na wimbi la watu, hususan watoto kupotea kwa wingi jijini Dar katika siku za hivi karibuni huku baadhi ya ndugu waliowahi kupotelewa na ndugu wakiibua vilio upya wakiamini ni miongoni mwa viungo hivyo.