Kijana Lawrent Lawrian, akiwa na uvimbe wa ajabu kichwani mwake.
Lawrent
Lawrian, 42 (pichani), ni mkazi wa Kijiji cha Nyakisogo, Wilaya ya
Biharamlo, mkoani Kagera, amekuwa mwenye huzuni na kukosa raha kwa muda
wa miaka 35 kutokana na gonjwa la ajabu linalomtesa ambalo
limemsababishia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutoendelea na masomo.
Gonjwa hilo la ajabu ni uvimbe kama nundu kichwani wenye uzito wa kilo 3, ulimuanza akiwa darasa la kwanza.
Akielezea zaidi kwa njia ya simu hivi karibuni Lawrent alisema: “Gonjwa
hili lilianza kama kauvimbe nikiwa na umri wa miaka saba, wakati huo
nilikuwa na wazazi wote na ilipofika mwaka 1992 baba akafariki dunia.
“Nikabakia
na mama tukawa tunaishi kwa kutegemea kilimo cha kawaida, nilikuwa
nikienda shule lakini ilifikia hatua nilishindwa kutokana na maumivu na
manyanyaso.
“Darasa
la saba nilimaliza kwa tabu sana, kwani wanafunzi wenzangu walikuwa
wakinicheka na kunitenga, licha ya kuadhibiwa na walimu lakini
hawakuacha tabia yao.
“Kutokana
na hali hiyo, nilishindwa kuendelea na masomo kwani nilikuwa
nikifungiwa ndani ili kunipunguzia kero toka kwa wenzangu.
Kijana Lawrent Lawrian akiuguza uvimbe.
“Nilikaa kwa kujificha hadi nilipojiona mkubwa nikaamua kuoa, sasa nina watoto sita wanaonitegemea.
“Kwa
upande wa matibabu baada ya uvimbe kuwa mkubwa nilipelekwa kwa padri
mmoja katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo lakini hawakugundua
tatizo kutokana na kutokuwa na vifaa vya kumpimia.
“Baadaye
kuna madaktari Wazungu walifika katika Hospitali ya Bukoba nikaenda,
waliponipima walisema ni uvimbe wa kawaida lakini hawakuweza kunitibu.
“Ilibidi
nikae nyumbani, maumivu yalizidi kuongezeka nikawa nashindwa kupata
usingizi, nikalazimika kwenda Hospitali ya Mgana, nilifanyiwa vipimo,
nao walisema ni uvimbe wa kawaida ambao unatakiwa ufanyiwe upasuaji na
nikaambiwa gharama yake ni shilingi milioni moja na laki sita,
nikashindwa kwa kuwa sina fedha hizo.
“Kwa
sasa uvimbe huu umekua mkubwa sana na ni mzito na umenifanya nishindwe
kwenda shambani, nimekuwa mtu wa kulala, familia yangu nayo inapata
shida.
“Mtoto
wangu wa kwanza kati ya sita yupo kidato cha pili na wote wamekuwa
wakimtegemea mama yao anayewatunza kwa kipato kidogo kinachopatikana
kutokana na kilimo cha jembe la mkono.
“Nawaomba
wasamaria wema wanisaidie kupata fedha za matibabu ili kuokoa maisha
yangu kwa kuwasiliana nami kwa namba 0714-533 430.”