MKONGWE wa muziki wa kizazi kipya, Lucas Mkenda ‘Mr
Nice’ ameibuka na kufunguka kuwa siri ya kufilisika kwake ni kupenda
kwake sifa kutoka kwa wapambe na matumizi mabaya ya fedha alizokuwa
akiziingiza.
“Enzi zangu nani asiyejua kuwa nilikuwa natembea na kundi la mabaunsa, mademu na kila kumbi nikiingia basi kila mtu atajua kama Nice yuko ndani lakini mwisho wa sifa zile ni nini? Si ndiyo zimenifikisha hapa nilipo.
“Nilikuwa na kila aina ya kamati ya ufundi, mashehe, wachungaji na maaskofu, wote walikuwa wangu, lakini kwa kuwa nilikuwa nataka sifa, dua zao zilikuwa kazi bure kwa sababu nilikuwa mtu wa starehe,” alisema Mr. Nice.
NENO LAKE KWA DIAMOND
Katika kile kinachoonekana kama kumuonya staa wa sasa anayekimbiza katika Bongo Fleva, Abdul Nasibu ‘Diamond’, alisema kwa kila ‘vurugu’ anayoifanya, yampasa kumtazama yeye kama mfano halisi endapo ataendekeza maisha ya anasa na kutaka sifa.
“Diamond kwa sasa anawika, anakubalika sana, ni kama ilivyokuwa kwangu. Namsihi asijisahau. Maisha yanabadilika. Namtakia mema ndiyo maana namshauri. Aachane na maisha ya kuwafurahisha watu, atengeneze maisha yake yajayo.
“Kuna wakati muziki unakataa, hapo ndipo mawekezo yake yatakapomfanya aendelee kuishi maisha bora bila muziki,” alisema Mr. Nice