NB-Picha haihusiani na habari hapa chini |
Vitendo vya baadhi ya wazazi, kudhalilisha walimu vinaendelea, ambapo mzazi mmoja Selemani Juma, amewashambulia walimu wawili kwa viboko.
Amefanya hivyo kupinga mwanawe kurudishwa nyumbani, akashone kaptura. Alifanya hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa
zilizomfikia mwandishi zilibainisha kuwa Juma alidhalilisha walimu
wawili wa Shule ya Msingi Nzogimlole iliyopo wilayani Nzega mkoani
Tabora.
Aliwashambulia kwa viboko, akipinga kitendo cha mwalimu mmojawapo, kumrudisha nyumbani mwanawe.
Mwandishi
alifika katika shule hiyo, yenye walimu tisa tu na kuzungumza na
Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel Josephat, ambaye alisema mwanafunzi
huyo, Shaaban Maziku anayesoma darasa la pili, alipeleka ujumbe tofauti
na alioagizwa na walimu kwa baba yake, hivyo kusababisha kadhia hiyo.
Kwa
mujibu wa Mwalimu Josephat, mwalimu aliyedhalilishwa (jina
limehifadhiwa), alikuwa akifundisha katika darasa hilo na alipomuona
mwanafunzi huyo kavaa kaptura iliyochanika vibaya, kiasi cha sehemu za
siri kuonekana, alimrudisha nyumbani kwenda kurekebisha sare yake.
Mwalimu
Josephat alisema mwalimu huyo wa kiume wa darasa la pili, alimwagiza
mwanafunzi wake aende kwa baba yake, akamuombe amsaidie kushona kaptura
hiyo.
‘’Mwalimu
hana kosa, kwani mtoto kaptura yake ilikuwa imechanika vibaya kiasi
cha sehemu zake za siri kuonekana… walimu hatupaswi tuwaache hivi
watoto, mwalimu alichofanya ni kumwambia akamwambie baba yake aishone
ile sare, lakini mambo hayakuwa hivyo,’’ alisema Mwalimu Josephat.
Akizungumza
kwa majonzi, Mwalimu Josephat alisema mtoto huyo alipofika nyumbani,
alimweleza baba yake kuwa mwalimu huyo, amechana kaptura hiyo na
amemwagiza arudi nyumbani kwenda kumwambia baba huyo aishone.
Ujumbe
huo unadaiwa kusababisha mzazi huyo, kufika shuleni na kuanza kutoa
lugha chafu dhidi ya mwalimu huyo na baadaye baba huyo alianza kutoa
kipigo.
Mwalimu
Josephat alidai kuwa baba huyo, alianza kutumia mawe kurusha kwa walimu
hao. Baadaye alitumia fimbo, kumchapa mwalimu huyo wa darasa la pili.
Hatua
hiyo inadaiwa ilisababisha mwalimu huyo, kupiga mayowe kuomba msaada.
Wananafunzi waliokuwa darasani, walitoka na kuanza kumsaidia kupiga
kelele za kuomba msaada.
Mayowe
hayo yalisaidia mwalimu mwenzake, Elias Kafiku kutoka ofisini kwa nia
ya kuamua ugomvi huo ili wazungumze kiofisi na kufikia muafaka. Lakini,
mwalimu huyo pia aliambulia kipigo.
Kutokana
na kipigo hicho, mwalimu huyo wa darasa la pili alipata majeraha na
kupelekwa zahanati ya kijiji, ambako alipatiwa huduma na kuruhusiwa
kurejea nyumbani.
Akizungumza
na mwandishi, mwalimu huyo wa darasa la pili alisema hali yake
inaendelea vizuri. Alisema sababu ya kupigwa na mzazi huyo, hazijui kwa
kuwa alitekeleza majukumu yake kama kawaida.
Akitoa
maoni yake kuhusu tukio hilo, Mwalimu Elizabeth Kafulila wa shule hiyo,
alisema tukio hilo limewatia hofu katika utendaji kazi, kutokana na
mzazi kuingilia majukumu ya walimu.
Mwalimu
Elizabeth aliwataka wazazi kujirekebisha na kushirikiana na walimu
katika kulea watoto wao, na wanapokuwa na malalamiko, wafuate taratibu
za kiofisi.
Kamanda
wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda alisema mzazi huyo
anashikiliwa kwa tuhuma za kupiga na kujeruhi vibaya na atafikishwa
mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Tukio
hilo limekumbushia tukio la mwaka 2009 ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya
ya Bukoba mkoani Kagera, Albert Mnali, aliamuru askari kucharaza bakora
walimu wa shule za msingi wa wilaya hiyo.
Mnali
anadaiwa aliwaamrisha askari Polisi kuwacharaza viboko walimu hao,
kutokana na kusababisha wanafunzi kufeli mitihani pamoja na pia
kuchelewa kazini.
Walimu walioripotiwa kuchapwa viboko na Mkuu huyo wa Wilaya ni wa shule za msingi za Katerero, Kanazi na Kasenene mkoani Kagera.
Walimu karibu nchi nzima, walilaani kitendo hicho, wakisema kimewadhalilisha na kimekiuka haki za binadamu.
Baadaye, Serikali ilichukua hatua ya kumstaafisha kazi Mkuu huyo wa Wilaya.