Watu wawili wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kushambulia gari la magereza kwa risasi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashitaka matatu.
Watuhumiwa
hao, Peter Mushi (36) dereva na Godlisten Mongi (40) ambaye hati ya
mashitaka imemtambulisha kwamba ni mhandisi, walipandishwa kizimbani
jana kwa mashitaka ya kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha na
shambulio la kudhuru mwili.
Wakili
wa Serikali, Matarasa Alungo alidai mbele ya Hakimu Anipha Mwingira
kwamba Julai 2 mwaka huu, maeneo ya Mikocheni karibu na Hospitali ya
Regency, Kinondoni, washitakiwa walikula njama kufanya uhalifu.
Alungo
alidai katika mashitaka ya pili Mushi na Mongi waliwavamia askari wa
magereza WP 481 CPL Dotto na Dorin Damas na kuwapiga kwa kutumia silaha
ya moto.
Katika
mashitaka ya tatu, alidai watuhumiwa hao walimshambulia kwa kumpiga
Dorin katika uso wake na kumsababishia maumivu mwilini.
Washitakiwa
walikana mashitaka hayo na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Walirudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana na kesi
itatajwa tena Agosti 8 mwaka huu.
Wakati huohuo, watuhumiwa Mushi na Mongi wamepandishwa tena kizimbani katika mahakama hiyo, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Mshitakiwa
wa tatu katika kesi hiyo, raia wa Burundi, Maulid Nkurunziza (23)
hakusomewa shitaka mahakamani hapo baada ya Wakili Musini Mussa kueleza
kuwa yupo gerezani na angefuatwa huko kusomewa shitaka lake.
Mussa
alidai mbele ya Hakimu Joyce Mushi kwamba, Mei 23 mwaka huu, maeneo ya
Kunduchi Silver Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa walimuua Edwin
Humphrey, dereva wa pikipiki.
Washitakiwa
wawili hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina
mamlaka kusikiliza kesi ya mauaji. Washitakiwa walirudishwa rumande hadi
Agosti 8 mwaka huu.