Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, limemhoji kwa saa kumi na moja binti aliyerubuniwa na kupelekwa China ambako kwa miezi mitatu alikuwa akitumikishwa kwenye madanguro nchini humo.
Siku chache zilizopita, Mwananchi liliandika
mfululizo, makala kuhusu msichana Munira Mathias, (si jina lake halisi)
aliyetumikishwa kwenye madanguro nchini China, baada ya kurubuniwa
kwamba alikuwa akipelekwa kufanya kazi kwenye hoteli kubwa.
Munira alisema baada ya taarifa zake kuandikwa Interpol walimtaka afike ofisini kwao kwa mahojiano. Mara ya
kwanza alihojiwa kwa saa saba na aliitwa tena mara ya pili na kuhojiwa
kwa saa tatu na nusu.
“Walinihoji jinsi safari yangu ilivyokuwa na namna
ambavyo wale wanawake waliotuchukua kutoka hapa (Tanzania) hadi China
na walivyosuka mipango ya kunisafirisha,” alisema.
Alisema: “Walikuwa wanataka kuendelea kufahamu kwa
kina jinsi nilivyosafirishwa na walionisafirisha, hata hivyo nimewapa
ushirikiano wa kutosha.”
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri ofisi yake kumhoji
Munira na kwamba lengo ni kufahamu kwa undani jinsi Watanzania
wanavyotumikishwa kwenye madanguro hayo, pamoja na kujua jinsi biashara
ya binadamu kati ya China na Tanzania inavyofanyika.
“Nia ilikuwa ni kujua namna wasichana
wanavyotolewa hapa na kupelekwa huko, lakini kikubwa ni kufanya kazi
yetu kukomesha biashara hiyo kimataifa,” alisema Babile.
Alisema siyo mara ya kwanza kwa Interpol kufanya
jitihada za kukomesha biashara ya binadamu na kwamba hatua zimekuwa
zikichukuliwa kila mara na siyo kwa Watanzania pekee, bali hata raia wa
kigeni wanaokuja nchini.
“Tunafanya hii operesheni mara kwa mara. Kwa
mfano, waliwahi kuletwa wanawake kutoka Nepal, walipofika hapa hati zao
za kusafiria zikafichwa na wale wanaowatumikisha na wakaanza kufanya
biashara ya ukahaba na baadaye kuwalipa wale waliowaleta,”alisema
Babile.
Alisema kitengo hicho kimewahi kuwarudisha wanawake kutoka China waliofika hapa nchini kwa nia ya kufanya biashara ya ukahaba.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Lucy Ngonyani ambaye
ndiye aliyemhoji Munira alisema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina
kuhusu tukio la binti huyo kupelekwa China na matukio mengine yenye
uhusiano au kufanana na hilo.
Atishiwa kifo
Wakati hayo yakiendelea, Munira amesema hatua yake ya kuweka
wazi ukatili aliofanyiwa China umemfanya aishi kwa shaka baada ya
kusikia kuwa wanawake wa Magomeni ambao anawataja kuhusika kumsafirisha
wanamsaka ili kumdhuru.
“Nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yangu mmoja
(jina linahifadhiwa) ambaye tulikuwa naye China, aliniambia wale mabosi
wetu wa China wamewapa taarifa wanawake wa Magomeni ili wakinipata
popote waniue,” alisema Munira.
Alisema alianza kuona dalili hizo tangu alipotua
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitoka China
kwani walikuwapo baadhi ya wanawake ambao walishiriki katika mipango ya
safari yake.
Alisema aligundua kuwa mawakala waliomsafirisha
wanamtafuta walipomfuata rafiki yake aliyemsindikiza na kuuliza ni wapi
anakoishi hivi sasa.
“Hali hiyo inanitia shaka sana na ndiyo maana naishi maisha ya kujificha hata vyombo vya usafiri wa umma situmii,” alisema.
Kutokana na tishio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema kituo hicho
kinaandaa taratibu za kumsaidia msichana huyo kisheria.
“Tumeshazungumza naye, kwa bahati mbaya leo (jana)
aliitwa mahali lakini ilikuwa aje hapa na tufanye mipango ya kumsaidia
kisheria,” alisema Dk Bisimba....
Alisema kituo hicho kinalaani biashara ya
usafirishaji wa binadamu na kuwataka wasichana wote waliowahi kufanyiwa
vitendo hivyo kuwa na ujasiri wa kusema ili sheria zichukuliwe dhidi ya
wahusika.
“Tulipambana mpaka sheria ya kudhibiti
usafirishaji wa binadamu ikatungwa, awali iliwekwa pamoja na ile Sheria
ya Makosa ya Kujamiiana lakini hivi sasa ni sheria inayojitegemea,”
alisema.
Taasisi nyingine iliyojitokeza kumsadia binti hiyo
ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ambacho
kimeahidi kukutana naye ili kuona jinsi ya kumsaidia.
Munira alipelekwa China katika Jimbo la Guangzhou
na kufanyishwa biashara ya ukahaba baada ya kurubuniwa kuwa anakwenda
kufanya kazi katika hoteli kubwa.
Pamoja na manyanyaso mengine, aliwahi kubakwa na
wanaume wanne wa Nigeria na kuambukizwa magonjwa ya zinaa pamoja na
kushika ujauzito ambao hata hivyo, ulitoka baadaye.
Pamoja na adha hizo, alikuwa akiwajibika kuwalipa mabosi wake Dola 200 za Marekani (Sh330,000) kila siku, kutokana na fedha azizokuwa akipata kwa kufanya ukahaba
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
Pamoja na adha hizo, alikuwa akiwajibika kuwalipa mabosi wake Dola 200 za Marekani (Sh330,000) kila siku, kutokana na fedha azizokuwa akipata kwa kufanya ukahaba
Chanzo: Gazeti la Mwananchi