Featured Posts

Friday, May 9, 2014

KAFULILA AWA MBOGO NA KUWALIPUA MAWAZIRI AKAUNTI YA ESCROW

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana aliibua tuhuma nzito bungeni akiwahusisha mawaziri wawili na Sh200 bilioni zilichotwa katika Akaunti ya Escrow, iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Katika tuhuma hizo, alimuunganisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wa Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
Mbunge huyo alisema fedha zilizoibwa katika Akaunti ya Escrow ni nyingi kuliko zile zilizoibwa katika kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT mwaka 2005.
“Pamoja na hilo, Watanzania wamekuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari kwamba Tanesco wakati ilipokuwa na mgogoro na IPTL walifika mahali wakafungua akaunti ya Escrow,” alisema.
Mbunge huyo alisema akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2004 na hadi jana, akaunti ile ilishafikia Dola za Marekani 122 milioni,” alisema Kafulila.
Alisema fedha hizo ziliwekwa kwa lengo maalumu kutokana na mgogoro uliokuwapo kati ya IPTL na Tanesco ili ziweze kusaidia malipo baada ya mgogoro kuisha katika Baraza la Usuluhishi wa Kibiashara la ISCID.
Alitaka jambo hilo liingie kwenye rekodi kwa kuwa linahusu BoT na vigogo akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu wake na pia Waziri wa Fedha.
Alisema wakati Tanesco ikidaiwa madeni zaidi ya Sh400 bilioni, viongozi hao wameidhinisha kugawanywa kwa fedha hizo kihuni jambo alilosema halivumiliki hata kidogo.
Kafulila alisema fedha hizo zilichotwa na Kampuni ya PAP aliyosema ya “Singasinga na ya kitapeli” ambayo iliidhinishiwa kuchota fedha hizo kinyume na utaratibu.

TUMEAMIA HUKU