Featured Posts

Tuesday, July 22, 2014

WANASWA NA MABOMU 7, RISASI 6, BARUTI JIJINI ARUSHA


Na Joseph Ngilisho, Arusha
JESHI la polisi hapa nchini limefanikiwa kuwatia mbaroni vinara wa milipuko ya mabomu hapa nchini, Yusufu Ally (30) na mkewe Sumaina Juma (19), wakazi wa Sombetini, wakiwa na mabomu ya kurusha kwa mkono aina ya Gurnet saba, risasi sita za shotgun, baruti, mapanga mawili na bisibisi moja.

Mabomu na risasi walizokutwa nazo Yusufu Ally na mkewe Sumaina Juma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, alisema kati ya mabomu hayo moja limetengenezwa nchini Ujerumani na sita yametengenezwa Urusi.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana saa 2 usiku katika eneo la Sombetini mjini hapa baada ya jeshi la polisi kupata taarifa juu ya watuhumiwa hao kuhusika na matukio ya milipuko ya mabomu.
Mtaalamu wa mabomu kutoka Jeshi la Polisi akionyesha kwa waandishi wa habari moja ya bomu lililokamatwa.
Aliongeza kuwa polisi inamtafuta kinara muhimu wa mabomu, Yahaya Hussen Hela (35), mkazi wa Mianzini jijini hapa, huku watuhumiwa wengine 25 akiwemo mfanyabiashara maarufu jijini hapa anayemiliki mabasi ya Kandahal Said Temba (42), pamoja na Imamu wa Msikiti wa Masjidi Qubia, Japhal Lema (38) ambaye pia ni mwalimu wa shule ya msingi wilayani Arumeru wakishikiliwa kuhusisana  matukio ya mabomu.
Miongoni mwa watuhumiwa hao, sita kati yao wanahusishwa na tukio la ulipuaji wa mgahawa wa Vama uliotokea Julai 7, mwaka huu,na kusababisha majeruhi wanane raia wenye asili ya Kiasia.
Watuhumiwa sita wa mlipuko huo wametajwa kuwa ni Shabani Hussen (38)ambaye alikuwa mlinzi katika mgahawa huo, Mohamed Nuru (30) mlinzi wa mgahawa wa jirani na tukio, Japhari Lema (38), Abdul Mohamed (31), wakala wa mabasi stand pamoja na Said Temba (42), wote wakazi wa jijini Arusha.
Mngulu alisisitiza kuwa polisi inaendelea kuwasaka wahuhumiwa wengine zaidi na kwamba jeshi hilo limeahidi kutoa zawadi kwa atakayeweza kutoa taarifa za siri zitakazowezesha kupatikana kwa wahusika hao.

TUMEAMIA HUKU