Featured Posts

Saturday, July 5, 2014

UNAZIJUA SIFA ZA KIONGOZI ANAEFAA KUTUONGOZA MWAKA 2015, SOMA NA UZIJUE HAPA


“Na mimi nashangaa kwa nini, kwa kweli nashangaa kabisa kutajwatajwa huku, wazee kama mimi na Salim (Dk Salim Ahmed Salim). Nini kimetokea katika nchi hii hata sisi tufikiriwe?” Jaji Joseph Warioba.

Dar es Salaam. 
 

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa dira ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kutaja sifa za rais anayefaa kuiongoza Tanzania. 

Warioba alisema kwamba taifa la Tanzania linastahili kuongozwa na vijana wenye nguvu ya mwili na akili. “Mimi nafikiri tuangalie kati ya vijana tulionao, nani anatufaa kuiongoza nchi, tusirudi kuangalia wazee,” alisema Jaji Warioba.


Alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika wiki hii ofisini kwake jijini Dar es Salaam.


Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja huku ukiwa umesalia takribani mwaka mmoja na miezi minne, kabla ya taifa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaoshirikisha vyama zaidi ya 23 vyenye usajili wa kudumu nchini.


Uchaguzi huo mkuu ambao ni wa tano wa vyama vingi nchini, unatarajiwa kulipatia taifa rais mpya, baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake wa utawala wa awamu ya nne.


Mbali na wagombea wa vyama vya upinzani, ndani ya CCM pekee kunatajwa kuwa na makundi zaidi ya manne yanayotarajia kuwania urais mwaka ujao.


Makundi hayo ni pamoja na linalotajwa kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, kundi lingine linatajwa kuwa nyuma ya Samuel Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na linalomuunga mkono Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, Stephen Wassira anatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.


Hata hivyo, viongozi hao wamekuwapo madarakani katika nyadhifa na nyakati tofauti huku pia wakiwa na umri uliovuka ujana, unaopendekezwa na Jaji Warioba.


Ndani ya CCM vijana wanaotajwa kutaka kuwania urais mwakani ni pamoja na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba.


Makamba tayari ametangaza nia yake ya kuwania urais akisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola, licha ya chama hicho kuzuia kutangaza nia na kupiga kampeni kabla ya muda.


Makamba, mmoja wa makada wa CCM walioonywa na chama hicho baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, alijipigia debe kuwa iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye vipaumbele vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora. Akizungumzia uzoefu Makamba alisema hakuna ushahidi wowote kwamba miaka mingi kwenye siasa ndiyo inatengeneza kiongozi mzuri.


“Uongozi mzuri unatengenezwa na haiba, wajihi, dhamira, uwezo, maadili, uhodari, hekima na maarifa. Sifa hizi hazipatikani kutokana na uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa hata baadhi ya vijana wanazo,” alisema Makamba.


Alitolea mifano mingi duniani ambapo vijana ambao hawakuwa na uzoefu kabisa katika nafasi za siasa wameshinda na kubadilisha nchi kama Tony Blair wakati anakuwa Waziri Mkuu wa Uingereza aliongoza nchi hiyo kubwa wakati alikuwa hajawahi kuwa hata Naibu Waziri.


“Barack Obama (Rais wa Marekani) alikuwa Seneta miaka mitatu tu, Julius Nyerere alikuwa Mwalimu akaingia siasa akaja kupewa uongozi wa nchi akiwa na miaka 39 tu.”


Hata hivyo, Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM iliwapa onyo kali makada wake sita akiwamo January Makamba ikiwatuhumu kupiga kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.


Katika maelezo yake Jaji Warioba alisema kwamba tangu uhuru, walioshika madaraka ya kuliongoza taifa walikuwa ni vijana.


Wazee kugombea urais. 
Akijibu swali kama atakuwa tayari wananchi wakimtaka kuwania urais baada ya kazi kubwa ya kukamilisha Rasimu ya Katiba nchini, Jaji Warioba alisema:


“Hili nilikwishalijibu, tusahau mawazo kwamba sisi (wazee) tutarudi madarakani. Nadhani mara ya mwisho tulipozungumza niliwaambia inafika wakati kiongozi unang’atuka. Unawaachia vijana ambao wana nguvu ya kimwili na akili ndiyo watumikie taifa hili, waongoze nchi.


“Na mimi nashangaa kwa nini, kwa kweli nashangaa kabisa kutajwatajwa huku, wazee kama mimi na Salim (Dk Salim Ahmed Salim). Nini kimetokea katika nchi hii hata sisi tufikiriwe?” alihoji Jaji Warioba.


Alisema kuwa tangu uhuru hadi sasa Tanzania imetayarisha vijana wengi wanaofaa kuliongoza taifa na kuongeza:


“Hatuna ombwe la uongozi, tunao vijana wengi sana, tena kwa bahati nzuri nchi kwa kiwango kikubwa ilikuwa ikiongozwa na vijana.”


Huku akitaja mifano ya viongozi hao vijana walioongoza taifa, Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema:


“Tulipoanza Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa nchi hii, alikuwa kijana. Alikuwa hajafika hata miaka 40, hata wenzake walikuwa vijana. Vijana ambao hawakuwa na uzoefu wa kuendesha Serikali, waliichukua nchi.”


Mwanasheria huyo mkongwe aliyelitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali alieleza kuwa hata waliofuata katika kulitumikia taifa walikuwa vijana.


“…Waliofuata, walioshika nafasi za kuitumikia nchi hii tuliwaona, walikuwa vijana. Edward Sokoine (aliyekuwa Waziri Mkuu), aliingia akiwa bado kijana, akastaafu bado kijana, bahati mbaya akafariki akiwa pia bado kijana. Dk Salim aliingia na miaka 42, mimi nilikuwa na 45, Sumaye aliingia bado akiwa kijana,” alisema Jaji mstaafu Warioba huku akihoji tena: “Hivi kimetokea nini sasa tunaanza kuangalia wazee…, nini kimetokea nchi hii tuanze kufikiria wazee?”


Jaji Warioba alipoulizwa kati ya vijana walio kwenye uongozi, yupi atafaa kuongoza taifa alisema:


“Sitaki, sitaki majina, … ni sifa. Sifa zipo, hebu mchukue alizotaja Mwalimu Nyerere mwaka 1995. Tunataka kiongozi mwenye maadili, mwenye ‘commitment’ (kuwajibika),ambaye atasimamia, ataapa kuisimamia Katiba.”


Makundi ya urais 
Warioba pia aliulizwa iwapo makundi yanayotajwa kusaka urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 kuwa huenda yanahusika na kusuasua kwa Mchakato wa Katiba Mpya.


Alisema kwamba, yeye na wenzake waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu na kutafakari mchakato huo unavyokwenda ukihusisha maeneo na makundi mbalimbali.


“Tulikwenda kutafakari, hatutaki kwenda kwenye matukio, wala kuzungumzia makundi, nasema wote wakae pamoja waone masilahi ya taifa, kwa sababu wasipokaa pamoja kuna hatari ya mchakato huu wa Katiba Mpya kukwama. Na kukwama siyo kwa masilahi ya taifa,”alisema.


Ikiwa Rasimu ya Katiba Mpya itapitishwa na mapendekezo yake ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu, kutalazimika kuwapo kwa Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo nguvu na mfumo wa kisiasa kubadilika.MWANANCHI

TUMEAMIA HUKU