Akizungumza na paparazi mwishoni mwa
wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI)
Isaya Mngulu alisema kuwa mtu huyo anasakwa kwa kuwa anatenda kosa la
jinai.
“Kutumia mtandao kujifanya wewe ni mtu
fulani wakati siyo ni kosa la jinai, hivyo tunamtafuta ili achukuliwe
hatia za kisheria,” alisema DCI Mngulu.
Mngulu alikuwa akijibu maswali ya
waandishi wetu waliofanya uchunguzi na kugundua kuwa kuna mtu anatumia
mtandao wa Twitter kujifanya ni Balali na kukanusha kuwa hajafariki
dunia.
paparazi walitaka kujua kwa DCI hatua
za serikali kwa mtu huyo ambaye huwa anaandika kwenye mtandao wa Twitter
kuwa aliwahi kuonana na Rais Jakaya Kikwete nchini Marekani na kufanya
mazungumzo.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI) Isaya Mngulu.
Mtu huyo hakuishia hapo kwani hata hivi
karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilipochapisha kaburi la Balali
lililopo Washington DC aliibuka na kukanusha kuwa yeye hajafa na
kuzikwa.
“Naomba hizo nakala zake za alivyotwit
ili tuzifanyie kazi,” alisema DCI Mngulu baada ya kuoneshwa nakala za
maelezo ya Balali feki kwenye mtandao.
DCI alipewa nakala hizo na waandishi wetu na kuahidi kumsaka mtu huyo.
Naye Afisa wa Mawasiliano Mkuu wa
Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Semu Mwakyanjala alipofuatwa
ofisini kwake na waandishi wetu na kuelezwa kuhusiana na Balali huyo
feki alisema anachokifanya mtu huyo ni kitendo cha kihalifu.
“Ukweli ni huo kwamba anatenda uhalifu
na polisi watakapohitaji mambo ya kitaalamu kuhusiana na suala hilo
tutatoa ushirikiano ili mtu huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria,”
alisema Mwakyanjala.
Balali, alifariki dunia Mei 16, 2008
huko Boston, nchini Marekani, wakati ambao alikuwa akiaminika kuwa
shahidi muhimu wa kashfa ya wizi wa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa
kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Tangu wakati huo hadi sasa tunapoandika
habari ya Balali feki, kumekuwa na kauli zinazoashiria kuwapo hali ya
kutiliwa shaka kuhusu ukweli wa kifo chake, na bila shaka mtu huyo
anayejifanya ni Balali anaitesa na kuikasirisha familia yake.