Watafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi
na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya
Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi
kupatikana katika tafiti za awali duniani.
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili
aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa
tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi
kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na
hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa
hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni
tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa
kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje
yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli
(CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika
kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia
wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu
na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4,
hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha kutumia
dawa.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC),
Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika
teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama imepatikana teknolojia ya
kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili
lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi
kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu
kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini
hilo likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo
(inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani
ya mwili. Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza
kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi
zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.