Featured Posts

Monday, September 22, 2014

MKE WA KIGOGO MKUBWA ATIWA MBARONI KWA WIZI SUGU WA MAGARI

Nuru Ramadhani Nasibu (pichani), mkazi wa jijini Dar es Salaam aliyekuwa akitafutwa na polisi wa nchini na wa kimataifa (Interpol) kwa kuhusishwa na wizi wa kuaminiwa wa magari matatu mali ya Dk. Emmanuel Matech  ametiwa mbaroni.
Nuru Ramadhani Nasibu, mkazi wa jijini Dar es Salaam anayetuhumiwa kwa wizi wa magari.
Taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi hilo juzi zinadai mwanamke huyo alitiwa mbaroni hivi karibuni na kwa sasa jalada la kesi yake linaandaliwa kwenda kwa mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP) kwa hiyo yupo nje kwa dhamana.
Kabla ya kutiwa mbaroni kwa mwanamke huyo ambaye ni mke wa kigogo wa ulinzi wa kampuni ya taasisi moja ya umma nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kupitia ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai liliandika barua Julai 13, mwaka huu iliyokuwa na namba ya jalada OB/IR/5705//2014 wizi wa kuaminiwa.
Katika barua hiyo, magari matatu yalitajwa kuibwa kwa kuaminiwa na mwanamke huyo ambayo ni Toyota Harrier (namba T 948 CGV), Toyota Prado (T 928 CJS) na Toyota Rav 4 (T 673 BXR) na mtuhumiwa ametajwa kwamba ni Nuru ambaye alikuwa bado hajakamatwa.
Hili ni moja ya gari analodaiwa kuiba
Tangazo la kumsaka mwanamke huyo lilitolewa baada ya Dk. Matech kutoa taarifa polisi na kufungua kesi yenye jalada namba OB/RB/10649/2014 wizi wa kuaminika, mtuhumiwa akiwa Nuru.Mwandishi wa habari hii alimtafuta mmiliki huyo ambaye katika mahojiano alikiri kuwa magari hayo ni yake lakini Nuru alikwenda kwake Januari, mwaka huu na kukodisha kwa awamu tofauti ambapo awali alilipa na aliamini angeyarudisha kwa muda waliokubaliana lakini hakufanya hivyo.
“Kilichoniumiza moyo ni pale nilipomfuatilia ili anilipe fedha zangu na magari yangu, alinipa cheki ya Februari 8, mwaka huu, ya shilingi milioni tano, kwenda Benki ya NMB lakini katika akaunti yake hakukuwa na fedha ya kufikia kiasi hicho.“Nilipomfuatilia alisema atanilipa nisiwe na hofu, lakini cha kushangaza ni kwamba gari moja Rav 4 ameweka bondi kwa Dk. Mnyau kwa kipindi kirefu na alishindwa kulikomboa kwa sababu hajalipa fedha,” alisema Dk. Matech.
Mwandishi wetu alimtafuta Dk. Mnyau kutaka kujua kama ana gari hilo ambapo alikiri na kusema Nuru alimkopesha fedha na kuweka gari hilo bondi lakini hajarejesha fedha hizo hivyo si rahisi kumpa gari.
“Julai 25, mwaka huu, nilimfungulia kesi namba 8485/2014 yeye na mume wake, Ramadhani katika Mahakama ya Mwanzo Manzese/Sinza kwa sababu wote nawadai shilingi milioni 12 walizonikopa kwa nyakati tofauti kwa kutegemea gari hili lakini mpaka sasa hawajalipa,” alisema Dk. Mnyau.
Aliendelea kudai kwamba pamoja na kupeleka kesi mahakamani, Agosti 5, 13, 19, 29 na Septemba 9, mwaka huu hawajakanyaga mahakamani, kesi hiyo ipo chini ya Mhe. Zaginga Patrick.
Mwandishi wa habari hii aliwatafuta Nuru na mumewe kwa njia ya simu lakini simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa na alipowatumia ujumbe kuhusiana na suala hilo mume wake alijibu hivi:
“Wewe andika unachojua, mimi siwezi kuzungumzia jambo wakati vyombo vya sheria vinashughulikia.”

TUMEAMIA HUKU