Stori: Musa Mateja
NYOTA
wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye hivi karibuni
aliripotiwa kupokea kipigo cha maana kutoka kwa msanii mwenzake, Rashid
Makwilo almaarufu Chid Benz, ameibuka na kudai kuwa atahakikisha rapa
huyo anaozea jela kwa kitendo hicho alichomfanyia.
“Chid na mama yake wamenipigia simu kutaka nimsamehe lakini ninashindwa kwa sababu akiulizwa na watu anakataa hajanipiga, sasa kama hajanipiga anaomba msamaha wa nini, nimekwenda kwao na polisi kama mara tano lakini haonekani, inaonekana amejificha sehemu, mimi nasema awaonee haohao wasiojua sheria,” alisema msanii huyo ambaye hivi sasa anaendesha vita dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Chid Benz mwenye tuzo tano za Kili, licha ya kukiri kumpigia Ray C simu pamoja na mama yake, alikataa kupiga kwa ajili ya kuomba msamaha kwa sababu hakumpiga msichana huyo mkongwe katika Bongo Fleva.
“Mimi nimpige Ray C? Halafu achubuke mguuni? Chid Benz angempiga angepasuka sura na angevimba kila sehemu. Yeye anajua nini kilitokea lakini anasema maneno yasiyokuwepo ilimradi apate huruma ya watu. Nilishamkataza kuwa karibu na mzazi mwenzangu kwa kuwa najua kampuni yake haina future.
“Mbona hasemi kama nilishawahi kwenda pale na kumweleza sitaki na akaniomba msamaha?
“Mimi sikumpiga, mchubuko alioupata ni mchecheto wake tu baada ya kujikwaa na kuanguka wakati akinikimbia, mimi nichukue cheni? Hayo ni mambo ya kizamani kwamba mtu ukimpatia sababu unasema amechukua pesa sijui na nini, siwezi kuchukua cheni ya Ray C, kwa maisha gani aliyonayo?
“Anasema nilimpigia simu kumuomba radhi, ni kweli lakini siyo kumwomba radhi, nilimpigia na kumwambia tuachane na haya mambo, sisi wote tunaonekana mateja tu mbele za watu ambao tumeshindwana huko sasa tunataka publicity.
“Wanaosema mimi ni mkorofi hawanijui, kama ni hivyo mbona ile kesi ya kumpiga msichana kule Ilala nimeshinda?” alihoji Chid Benz.