WAUMINI wa dini ya Kiislamu kote duniani, hivi sasa wapo katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambao hutokea kila mwaka, kuelekea Sikukuu ya Idd el Fitr. Ni siku zipatazo 30 ambazo Waislamu wanatakiwa kuacha kutenda dhambi, sambamba na kufunga kula chakula nyakati za mchana.
Ingawa siku zote za maisha yetu hapa duniani tunatakiwa kuacha kutenda dhambi, kufanya mambo ya kumpendeza Mungu na kuwa watu wema, lakini mwezi huu umefanywa kuwa maalum zaidi na uzoefu wa kimazingira unaonyesha kuwa matendo maovu kama wizi, ubakaji, biashara ya uchangudoa na uhalifu mwingine hupungua kwa kiwango kikubwa.
Kupungua kwa matukio ya kihalifu na ukosefu wa maadili wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unathibitisha kitu kimoja kuwa, kama binadamu, tunao uwezo wa kujizuia kufanya matendo maovu, lakini huenda ni kwa vile tunao udhaifu mkubwa wa kibinadamu, unaotufanya tujikute tukipotoka.
Ingawa ujumbe huu ni kwa watu wote, ndugu zangu Waislamu na wasio Waislamu, lakini ni maalum zaidi kwa mastaa wetu wa fani mbalimbali, kuanzia wanamichezo na wasanii, kwa sababu wao ndiyo wanaoiwakilisha jamii inayowazunguka.
Kuna msemo unaosema msanii ni kioo cha jamii. Sina uhakika kama wasanii wenyewe wanajua nini maana ya msemo huu. Kwa kuwasaidia, huu ni msemo wenye maana kubwa sana kwao kwani wote tunajua kioo kilivyo, ukijiangalia unajiona.
Huwezi kujitazama halafu ukajiona tofauti na ulivyo.
Tunaposema wao ni kioo cha jamii, tunamaanisha tukiwatazama, jinsi wanavyoishi, wanavyozungumza, wanavyovaa na kila wanachokifanya, basi hivyo ndivyo jamii yao ilivyo.
Tunaposema wao ni kioo cha jamii, tunamaanisha tukiwatazama, jinsi wanavyoishi, wanavyozungumza, wanavyovaa na kila wanachokifanya, basi hivyo ndivyo jamii yao ilivyo.
Lakini matendo ya baadhi ya wasanii wetu, jinsi wanavyovaa mavazi yao ya nusu utupu, wale akina kaka wanaovaa chini ya makalio, akina dada wanaosagana, wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wanaotumia madawa ya kulevya na mambo mengine yasiyo na maadili, hayawakilishi taswira halisi ya Mtanzania tunayemfahamu.
Ni kwa sababu hiyo, nilipenda kuwashauri vijana wetu mastaa, kuzingatia maadili yetu yanavyotuambia, angalau kwa kipindi hiki cha siku 30 tu ambazo tunawasindikiza ndugu zetu Waislamu kukamilisha moja kati ya nguzo kuu tano.
Itashangaza, kwa mfano, kusikia msanii mmoja mwenye mwili mkakamavu, amempiga binti mrembo mangumi baada ya kuwa amezidisha dozi ya sigara zao za kikubwa na wala hatutegemei kusikia eti watu wamekutana klabu na kuamua kupigana baada ya kulewa.
Ni wakati wa kujiangalia upya na kuchuja baadhi ya matendo ambayo hayampendezi Mungu, ili aweze kuwapa rehema, afya, nguvu na hata akili ya kuweza kuyapeleka maisha yao katika njia inayostahili. Wasanii wetu wengi, pamoja na fursa nyingi wanazokutana nazo katika harakati za kazi zao, bado wamekuwa hawana mipango madhubuti ya namna ya kujiweka vizuri kwa ajili ya kesho.
Ni kwa sababu ya kuendekeza starehe na mambo yasiyofaa, ndiyo maana wanakosa muda wa kutafakari. Hii ndiyo inayosababisha kusikika kwa habari nyingi zinazozalishwa nao mara kwa mara, lakini hasa zikiwaonyesha upande ule ambao wazazi wasingependa kusikia.
Kama ni lazima twende klabu usiku na kwamba hatuwezi kulala bila kupasha, basi siyo jambo baya kupunguza kiasi cha kiburudisho unachotumia, ili kutoa nafasi kubwa ya kutojikuta ukigeuka habari. Huu uwe ni mwezi ambao unaweza kubadili kabisa maisha yetu.
Binadamu huishi kwa kujifunza na huwezi kubadili maisha yako kama huwezi kubadili baadhi ya tabia. Wengi wanafanya mambo kwa sababu ya kutaka sifa, kuogopa kuonekana wamefulia au kuiga. Huu ni ujinga.
Kama umetumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kwenda kula maisha katika klabu za usiku kwa miaka mingi, hujachelewa kama sasa utasitisha safari hizo mwezi huu ili ujikague uone kama utakuwa umefanya jambo la maana au la!