Shule
ya Sekondari Mwadui iliyopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga,
imetangaza kufukuza wanafunzi wote wanaotumia vipodozi, wanaovaa sketi
fupi, milegezo na wanaotumia simu za mkononi shuleni.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria,
Mchungaji Yohana Nzelu, alisema hayo jana katika kikao cha Bodi ya Shule
na Wazazi.
Mwalimu
Nzelu alisema moja ya chachu ya mafanikio ya wanafunzi shuleni, ni
nidhamu ya kutosha na maadili mema na kuongeza kuwa Bodi hiyo ilikaa na
kujadili namna ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wake na kuweka mikakati,
ikiwemo hatua hizo.
Akisoma
taarifa kwa wazazi na walezi wa wanafunzi walio katika shule hiyo,
Mwalimu Nzelu alisema hatua hizo zinalenga kuzuia wanafunzi kujiingiza
katika makundi mabaya na kuboresha taaluma.
‘’Shule
hii katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012,
wanafunzi 61 waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu na mwanafunzi
mmoja alichaguliwa kwenda kidato cha tano.”
‘’Mwaka
jana (2013) wanafunzi 76 walifanya mtihani wa kidato cha nne, waliopata
daraja la kwanza mpaka la tatu 33, waliochaguliwa na Serikali kujiunga
kidato cha tano wanafunzi 24, na waliokwenda shule binafsi walikuwa
saba.
“Tumepiga hatua hivyo mikakati iliyopo ni kusisitiza maadili na kuondoa changamoto zilizokuwepo za wanafunzi kukosa nidhamu,“ alieleza Mwalimu Nzelu.
Akizungumza
kwenye kikao hicho, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi hiyo, Emmanuel
Makala, ambaye ndiye msimamizi wa shule hiyo, alisema suala hilo si la
kupuuzwa na hawatakuwa na msamaha kwa mwanafuzi atakayekiuka sheria hizo
huku akitoa mwito kwa wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja.