MKAZI wa Yombo Kilakala jijini Dar es Salaam, Charles Swai (48), amekutwa chumbani kwake akiwa amefariki dunia.Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP),
Englibert Kiondo, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 8:00
mchana, ambapo mwili wa marehemu ulikutwa kitandani na haukuwa na jeraha
lolote.
Kiondo alisema kifo hicho
kiligundulika baada ya Swai kutofungua mlango wa chumba chake tangu
alipofunga Julai 23 saa 2 usiku, ndipo majirani walipochungulia
dirishani na kumuona akiwa amelala na kutoa taarifa Kituo cha Polisi
Chang’ombe.Alisema askari walifika eneo hilo na kuvunja mlango na
kumkuta akiwa amefariki dunia. Chanzo cha kifo hakijafahamika na mwili
umehifadhiwa hospitali ya Temeke. Upelelezi unaendelea.
Katika tukio jingine, dereva
aliyefahamika kwa jina la Felix Mgoba (25) mkazi wa Wazo, amefariki
dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na
Fuso. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP), Camillius Wambura, alisema lilitokea
juzi saa 5:20 asubuhi huko barabara ya Bagamoyo eneo la Boko Msikitini.