Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi wa vyama vya siasa kukutana na kufikia makubaliano ili mchakato wa Katiba uendelee hatimaye kupatikana kwa Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Pia, Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu amemshauri Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuchukua hatua zitakazoondoa matatizo katika Bunge Maalumu la Katiba ili kuwezesha mchakato huo kukamilika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema ni muhimu viongozi hao kuweka kando tofauti zao za mawazo na mitizamo ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya taifa.
Warioba ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, ameonya kwamba ikiwa viongozi hao hawataweka kando tofauti zao na kuwezesha Taifa kupata Katiba Mpya, amani ya Taifa inaweza kuvurugika.
“Tunatoa wito kwa viongozi wa vyama wakutane watafakari hali ilivyo na kufikia makubaliano ili mchakato uendelee. Tunafikiri ni jambo bora wakarudi na usiwepo mjadala wa kuangalia idadi ya kura katika kufikia uamuzi, lengo lisiwe idadi ya kura, bali makubaliano ya kupata Katiba Mpya,” alisema jaji Warioba na kubainisha:
“Kipindi chote, sisi tuliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tulikuwa tukifuatilia kwa karibu sana mchakato unavyoendelea. Sisi ni wadau wakubwa, tulitumia miaka miwili kwa maandalizi, tuna hamu kubwa na matumaini ya kuona sasa Katiba Mpya inapatikana.”
Rais Kikwete na Dk Shein
Jaji Warioba alisema Rais Kikwete ndiye aliyeanzisha mchakato wa Katiba Mpya kwa nia njema na kwamba muda wote amekuwa akifanya kazi ya kuusimamia mchakato huo pamoja na kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba akishirikiana kwa karibu na Dk Shein, hivyo bado wana wajibu wa kuchukua hatua ili kukamilisha safari ya kupata Katiba.
“Sasa Bunge la Katiba lina matatizo, bado ni wajibu wao (Rais Kikwete na Dk Shein), kuchukua hatua ili kupata Katiba Mpya. Huu ni mchakato, awamu ya kwanza Bunge lilitunga sheria, ya pili Tume ya Katiba ikafanya kazi, ya tatu Bunge Maalumu la Katiba na nne wananchi watapiga kura. Mawazo yetu ni kusaidia mchakato huu ukamilike. Tunataka ufanikiwe,” alisema akionya:
“Tusije tukajidanganya kama tusipofanikiwa tutaendelea kwa usalama, kuna hatari ya amani ya nchi na usalama kuvurugika. Viongozi lazima waelewe hili kwani madai ya Katiba Mpya yalikuwapo zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Wananchi wengi wanaamini kuna umuhimu wa kupata Katiba Mpya, tena wengi wa hali ya chini, ingawa viongozi ndiyo walioanzisha madai hayo.”
Kauli hiyo ya Warioba imekuja huku maandalizi ya kikao cha Bunge la Katiba linalotarajiwa kuanza tena vikao vyake Agosti tano yakiendelea.
Aprili 16, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka kwenye Bunge la Katiba akilalamikia CCM kutowatendea haki kwa mambo mbalimbali ikiwamo kupinga mapendekezo yao hata ya msingi, akisema hawawezi kuwa sehemu ya watu wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya kuibomoa nchi.
Siku chache baadaye, walianza kufanya mikutano nchi nzima kwa kile walichodai kuwaeleza wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kuzunguka nchi nzima kueleza msimamo wake na sababu za wao kutaka kuendelea kutumika kwa muundo wa Serikali mbili unaotumika sasa na kubeza hoja za Ukawa.
Lakini jana Warioba alisema yeye na waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya walifuatilia hali ilivyokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba na baada ya kuahirishwa... “Tukaamua tukutane kwa siku tatu kama raia na kufanya tathmini kama raia, pia tuliamua kukaribisha wasomi na baadhi ya wabunge wa Bunge la Katiba. Tuliwaalika wasomi watano na wabunge wawili wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru na Profesa Abdul Sharif wa Zanzibar.
“Baada ya kuwasikiliza, tukafanya tafsiri yetu wenyewe na kufikia mahali tukasema ni muhimu jukumu la Bunge Maalumu la Katiba kuendelea. Liendelee kwa msingi wa kuimarisha mchakato wa Katiba Mpya, walifahamu hili, wafikie makubaliano.
“Waangalie wapi wanatofautiana, wapi wanakwenda sawa, waweke kando tofauti watoke na yanayowapatanisha ili kupata matokeo ya kuwa na Katiba Mpya.”
Serikali mbili au tatu
Jaji Warioba alisema kipindi kilichopita Bunge hilo lilishughulikia kanuni na kujikita zaidi katika mjadala wa muundo wa Serikali mbili au tatu, mambo yaliyochukua muda zaidi, lakini mkutano ujao utakuwa na mambo mengi zaidi.
“Muundo wa serikali mbili au tatu huo ulikuwa ndiyo mjadala. Katika eneo hilo hata bunge lijalo kazi bado kubwa inahitajika. Tunaweza kuzungumzia upungufu wa Serikali tatu, lakini bado kuna umuhimu wa kuzungumzia udhaifu wa Serikali mbili:
“Bado matatizo ya Tanganyika kuvaa koti la muungano, mgongano wa Katiba ya Zanzibar na Muungano, hatuwezi kunyamaza tukaamini yataondoka. Pia lipo suala la maadili na miiko ya viongozi,” alisema.
Warioba aliyefanya kazi katika Serikali tangu Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, alitaja mambo mengine muhimu kuangaliwa katika Bunge hilo kuwa ni utengano wa mihimili akisema lina mtizamo tofauti, madaraka ya rais, ukomo wa uongozi na madaraka ya wananchi kuweka au kuondoa mbunge madarakani, Tume huru ya uchaguzi, Tume ya Haki za Binadamu na suala la mgombea binafsi.