Featured Posts

Tuesday, July 1, 2014

waziri mkuu pinda adai Ukawa imeuweka njiapanda uchaguzi mitaa


Tanga. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema hatima ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea uamuzi wa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea katika Bunge Maalumu kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Pinda alisema hayo jana katika kikao chake na mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini uliofanyika hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa.
“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu umegubikwa na kitendawili kutokana na wajumbe wa Bunge hilo kugawanyika na kushindwa kufanya kazi waliyopewa kwa wakati ili Katiba iweze kupatikana mapema.
“Ni kama kitendawili kidogo kwa sababu bado Bunge la Katiba wanavutana. Tuna changamoto hiyo, tunaendelea kumwomba Mungu ili Ukawa waondoe hasira warejee bungeni,” alisema Pinda.
Hata hivyo, alisema ofisi yake inajiweka tayari kwa uchaguzi huo mwaka huu kama ulivyopangwa na kwamba hata kama utasogezwa, mipango iwe imeandaliwa na kuwa tayari kwa wakati wowote.
Alisema hata kama itatokea vinginevyo, Serikali kwa upande wake haikatazwi kuendelea kufanya maandalizi, ndiyo maana ofisi yake iko kwenye pilikapilika za kuweka mambo tayari kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo.
“Sisi tunakwenda na yote mawili, kama utakuwapo mwaka huu na hata kama utasogezwa mbele kwa sababu tusipofanya maandalizi nyie wenyewe mtakuja kunigeuka,” alisema Pinda.
Kauli hiyo ya Pinda imekuja wakati viongozi wa Ukawa wakisisitiza kuwa hawatarudi bungeni hadi pale watakapothibitishiwa kuwa Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa ni ile iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe wa Ukawa ambao ni wajumbe wa bunge hilo kutoka vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia bunge hilo wakidai kuwa wenzao wa CCM walikuwa wanataka kuingiza rasimu mpya inayoendana na mfumo wa Serikali mbili badala ya rasimu ya Tume iliyopendekeza serikali tatu.
Maandalizi ya uchaguzi
Waziri Mkuu alisema maandalizi ya uchaguzi huo  yanakwenda vizuri na kwamba hatua inayoendelea sasa ni uchambuzi wa maombi yaliyowasilishwa Tamisemi ya kuongezwa mitaa, vitongoji, vijiji na kata. Alisema hatua ya uchambuzi wa maombi ya vijiji, vitongoji, mitaa na kata mpya yapo mwishoni kabla ya kupitishwa rasmi na kupelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hatimaye kuingizwa kwenye orodha ya uchaguzi.
Pinda aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo jukumu la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Serikali Kuu ili kuwezesha Taifa kuwa na fedha za kujiendesha. “Katika hili sitakuwa na huruma kwa sababu bajeti ya safari hii tulishuka sana, halmashauri mlilala badala ya kutimiza wajibu wenu wa kukusanya mapato ipasavyo,” alisema Pinda.
Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanampelekea taarifa za kila miezi mitatu za kuelezea namna zilivyokusanya mapato na zionyeshe kuwa imefikiwa asilimia 100.

TUMEAMIA HUKU