Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
amejikuta katika wakati mgumu mbele ya
Rais Jakaya Kikwete baada ya kuzomewa
hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na
wananchi pamoja na madiwani wa CCM
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma
alipokuwa akitetea kuwapo kwa Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati
akijibu hoja za Mbunge wa Dodoma Mjini
(CCM), David Malole ambaye alitaka CDA
ivunjwe akiituhumu kuwavunjia
wananchi nyumba bila kuwatafutia
mahali pa kuishi.
Hoja ya Malole kutaka CDA ivunjwe
iliibuka katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kata ya Kikuyu,
Manispaa ya Dodoma baada ya Rais
Kikwete kuzindua ujenzi wa Barabara ya
Dodoma – Iringa.
Awali, mbunge huyo akitoa salamu kwa
Rais Kikwete, alisema CDA imekuwa ni
kero kwa wakazi wa mji huu.
“Mheshimiwa Rais, ni bora CDA ikafutwa na
ardhi ikarudishwa kwa halmashauri kwa
kuwa hakuna kitu kinachofanyika. Ipo miji
mingi ambayo haina CDA lakini imekuwa
majiji. Leo hii zaidi ya miaka 40 CDA
imeshindwa kuufanya Mji wa Dodoma kuwa
jiji,” alisema na kuongeza:
“Licha ya kuwa CDA jukumu lake ni
kuhakikisha inapima viwanja na kupanga
ustawi wa mji lakini imeshindwa kufanya
hivyo, jambo ambalo linawakera wananchi
wa Dodoma na kusababisha kukichukia
Chama Cha Mapinduzi na Serikali yao,”
alisema.
Kutokana na hoja hiyo kushangiliwa na
madiwani pamoja na wana CCM na
wananchi wengine, Malole aliendelea
kufafanua kuwa suala la kupigania
wananchi wapate viwanja linamuweka
katika hali ngumu kwa sababu anatishiwa
kuwa hatapata nafasi ya kugombea
ubunge tena.
“Mimi nasema, ikimpendeza Mungu kuwa
mbunge nitaendelea kuwa mbunge na
kama siyo mpango wa Mungu basi, kwani
kuna propaganda nyingi juu yangu lakini
hiyo yote ni kutokana na kupigania
wananchi wapewe haki zao,” alisema.
Kuzomewa
Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi
ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya CDA
alilazimika kupanda jukwaani ili
asawazishe kauli za mbunge huyo, jambo
ambalo liliibua zogo na wananchi
kuzomea.
Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala
katika kipindi chote alichokuwa jukwaani
huku viongozi wa chama wakihaha
kuwazuia wanachama na madiwani wa
CCM wasizomee bila mafanikio.
Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi
pale aliposema, “Mimi ni mdau mkubwa
wa CDA na ni kati ya watu ambao
walishiriki kupeleka maendeleo katika Mji
wa Dodoma.”
Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja
na wananchi kuanza upya kumzomea
huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa
madai kuwa hana cha kuwaeleza hadi
wamwelewe.
Hali hiyo iliambatana na nyimbo
zilizoanzishwa na madiwani, “CCM..
shuka chini, CCM shuka chini” hali
iliyomfanya Lukuvi kushuka jukwaani.
Baadaye Rais Kikwete akizungumza na
wakazi hao, alitoa siku saba kwa viongozi
wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge
kukaa na kutatua mgogoro huo na aliahidi
kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.
Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa
katika mikutano ya hadhara, bali vikao
vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia ni
jinsi gani watamaliza mgogoro huo bila
kuwa na fujo wala lawama.