Featured Posts

Monday, September 22, 2014

MAUZAUZA, MWALIMU AKUTWA AMEFUNGWA MINYORORO KANISANI

Ndugu wa mtu anayedaiwa kuwa ni mlemavu wa akili, Galus Focus Nguruwe (35) ambaye ni mwalimu wa sekondari moja mjini Morogoro, wamelituhumu Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship lililopo Boko Magengeni jijini Dar kuwa wamemfunga mnyororo ndugu yao huyo kwa miezi nane mfululizo.
Mwalimu Galus Focus Nguruwe akiwa amefungwa mnyororo
Kwa mujibu wa dada wa Galus, Piencia Focus, ndugu yao huyo alichukuliwa na mke wa mtoto wa dada yao waliyemtaja kwa jina la Doreen kutoka Songea mkoani Ruvuma Januari, mwaka huu bila kuwataarifu ndugu, jambo lililowafanya wamfuatilie na kugundua alipelekwa kwenye kanisa hilo kwa madai ya kufanyiwa maombi.
Dada wa Galus, Piencia Focus akiwa kanisani hapo
Dada huyo alisema kuwa aliamua kumtafuta ndugu yake hasa baada ya kupata taarifa kuwa aliko amekuwa akishinda  huku amefungwa mnyororo mguuni,  hali inayomfanya ajisaidie na kula papohapo.
“Japokuwa alikuwa na matatizo ya akili tangu zamani, lakini alikuwa akitumia dawa zake na alipata nafuu na kufanya kazi yake ya ualimu kwani alikuwa  akifundisha shule moja ya sekondari Morogoro,” alisema Piencia Focus.
Kaka wa Galus,Peter Focus akizungumza na waandishi wa habari.
Naye kaka wa Galus, aliyejitambulisha kwa jina la Peter alisema baada ya kupata taarifa kwamba mdogo wake yupo kwenye kanisa hilo aliamua kufika kwa ajili ya kumchukuwa kistaarabu lakini cha kushangaza alijikuta akiangukia kwenye mikono ya waumini hao wakidai yeye ni gaidi na wakamkwapulia fedha zake.
Peter alisema alipoachiwa alikimbilia Kituo cha Polisi Wazo Hill ambapo alifungua jalada lenye Namba za Kumbukumbu WH/RB/6364/14 WIZI TOKA MAUNGONI.
Waumini wa kanisa hilo wakijibizana na ndugu wa Galus kanisani hapo.
Peter alisema alilazimika kuungana na dada yake kwa kushirikisha na vyombo vya usalama ambapo walifika kanisani hapo kwa mara nyingine ili kumkomboa ndugu yao na kuwatia mikononi waumini waliomwibia fedha zake.
Waandishi wetu waliokuwa karibu na eneo hilo walizinyaka taarifa hizo na kufika kanisani hapo ambapo waliwashuhudia ndugu hao wakiwa na polisi wakimchukuwa mmoja wa watuhumiwa waliodaiwa kumshambulia Peter na kuondoka naye.
Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship kwa muonekano wa mbele.
Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kitendo cha polisi hao kumwacha Galus akiwa bado amefungwa kwenye nguzo na mnyororo kanisani hapo wakidai watamfuata baada ya kumpeleka mtuhumiwa wa unyang’anyi kituoni, jambo ambalo halikuwa la kweli kwani hawakufika kwa siku hiyo.
Waandishi wetu walishuhudia timbwili la aina yake kanisani hapo kati ya waumini wa kanisa hilo na ndugu wa Galus waliorejea kwa lengo la kumchukuwa ndugu yao baada ya awali kumpeleka kituoni mtuhumiwa wa kumshambulia Peter.
Waandishi wetu walipoomba kuzungumza na uongozi wa kanisa hilo ilishindikana na kujikuta wakishambuliwa kwa maneno huku wakitakiwa kuondoka mara moja katika eneo la kanisa hilo.

TUMEAMIA HUKU