Taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Nigeria zinadai kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Boko Haram, Abubakar Shekau ameuwa na majeshi ya Nigeria.
Tetesi hizo zilianza kusambaa Alhamisi iliyopita baada ya jeshi la Nigeria kutoa taarifa kupitia Twitter kuwa wamemjeruhi vibaya kiongozi wa ngazi za juu wa Boko Haram katika eneo la Konduga, Borno.
Wikendi iliyopita taarifa hizo zilianza kuaminika zaidi baada ya picha zinazoonesha mwili wa mtu anaeaminika kuwa Abubakar Shekau kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na tovuti mbalimbali.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Nigeria amekataa kuthibitisha taarifa hizo wala kuzikanusha akidai kuwa bado uchunguzi unaendelea.
“Katika point hii, sitaweza kuthibitisha au kukanusha taarifa hizi. Major General Chris Olukolade (Msemaji wa jeshi la Ulinzi) ataweza kutoa taarifa kuhusu hali hiyo hivi punde. Endeleeni kusubiri.” Msemaji wa jeshi la Nigeria, General Olajide Olaleye aliiambia AFP jana.
Jeshi la Nigeria linapata kigugumizi kuhusu taarifa hizo kwa kuwa miaka iliyopita waliwahi kutangaza kumuua Shekau na baadae akatokea na kutangaza uwepo wake kupitia kipande cha video.
July 30, 2009, kitengo cha ulinzi cha jiji la Maiduguri walieleza kuwa wamemuua Abubakar Shekau aliyekuwa msaidizi wa mwanzilishi wa Boko Haram, Mohammed Yusuf katika shambulizi lililosababisha vifo vya wapiganaji 200 wa kundi hilo.