Featured Posts

Saturday, September 6, 2014

Mgonjwa Aliyekuwa Akiombewa Kanisa la Gwajima Akutwa Amefariki Gesti

Habari mbaya inamhusu mwanamke aliyetajwa kwa
jina moja la Averina ambaye alikuwa akiombewa
kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima la Nabii
Josephat Gwajima ambaye anadaiwa kufia nyumba
ya kulala wageni (gesti) ya My Fair iliyopo Kawe
jijini Dar.
Tukio hilo lililoacha viulizo na kuzua minong’ono
midomoni mwa wengi lilijiri hivi karibuni ambapo
mwanadada huyo aligundulika kuwa amefia
chumbani mishale ya saa 4:00 asubuhi.
Akizungumzia tukio hilo, mlinzi wa gesti hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Haruni alisema,
mwanamke huyo alifikishwa mahali hapo
akionekana dhaifu kiafya, jambo lililosababisha
kumuhoji mtu aliyemfikisha hapo kuwa ni kipi
kimemsibu.
“Huyu dada alipofikishwa hapa na mtu
ninayemfahamu ambaye nasali naye kanisa moja la
Sabato, nikalazimika kumuhoji mama huyo
aliyemleta ana matatizo gani na kwa nini wamlaze
gesti wakati ni mgonjwa, ndipo akanipa mkasa
mzima.
“Aliniambia huyu mama hana makazi maalum na
alikuwa akisali kwa Gwajima na kulala uwanjani
hapo (Tanganyika Parkers, Kawe) huku hali yake
ikiwa si nzuri kiafya,” alisema mlinzi huyo.
Aliendelea kusema kwamba hadi kufikia uamuzi wa
kumlaza mahali hapo ni baada ya kuona hana
makazi huku akisaidiwa kupata matibabu.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa gesti hiyo,
Apolinary Shayo alisema siku ya tukio alipewa
taarifa kuwa kuna mtu amefia ndani na alipojaribu
kumuhoji mtu aliyekuwa ameenda naye kwa kuwa
alikuwepo mahali hapo kwa lengo la kumpelekea
chakula mgonjwa wake, akamueleza kuwa mama
huyo alikuwa akisumbuliwa na magonjwa tofauti
(hayakutajwa) kwa muda mrefu.
Mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa na polisi
wa Kituo cha Kawe, Dar kwa uchunguzi zaidi na
kutafuta ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi
ikidaiwa kwamba mama huyo alitokea mkoani
(haikujulikana ni mkoa gani).

TUMEAMIA HUKU