Mwinjilisti ambaye jina lake halikufahamika mara moja akikagua vifaa vya wachawi baada ya kuangushwa.
Tukio hilo la aina yake lilijiri usiku wa Mei 25, mwaka huu maeneo ya Tazara-Maghorofani, Dar hivyo kuibua hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo wakihofia kulogwa.
Habari zilieleza kwamba alfajiri ya siku ya tukio hilo, watu waliona matunguri kwenye uchochoro unaokatiza katika nyumba zao.
Watoto wakishuhudia tukio hilo.
Ilielezwa kwamba baadhi ya watu walidai kuwa matunguri hayo yalidondoshwa na wachawi waliopita eneo hilo wakielekea kuwaloga watu mahali fulani na kuongeza kuwa inawezekana kutokana na kanisa kuwa karibu na eneo hilo ndipo wakapata tafrani angani kiasi cha kudondosha rada zao.
Watoto wakizishangaa tunguri za wachawi.
“Hapa lazima wachawi walikuwa wanakwenda kuloga sehemu, lakini kutokana na kanisa kuwa karibu na njia zao wakajikuta wakipita kwa tabu. Mwishowe wakadondosha mizigo yao,” alisema mmoja wa mashuhuda.
Ilidaiwa kuwa umati uliofurika eneo hilo ulipatwa na wasiwasi na kutafuta msaada wa kiroho kwa kuwatafuta wachungaji wa kanisa hilo ambapo walikutana na wainjilisti wawili ambao walifika eneo la tukio na kuvikusanya vifaa hivyo kwenye kiroba huku wakiviombea.
Kuhusu maji meusi ilidaiwa kuwa hutumiwa na wachawi wasionekane wakiwa katika shughuli zao.
Wakizungumza na paparazi baada ya kuvikabidhi vifaa hivyo kanisani kwa ajili ya kuvichoma, wainjilisti hao waliojitambulisha kwa majina ya Amos Beda na Innocent Gervas wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) walisema kuwa, vifaa hivyo vinaonekana kuwa na uhusiano mkubwa na nguvu za giza.
Walimtaka mwenye navyo kujitokeza kanisani ili amrudie Mungu.