Featured Posts

Saturday, September 20, 2014

Azam Media Limited Wakabidhi Fungu La Pili Kwa Klabu Za Ligi Kuu TZ bara

Kampuni ya Azam Media Limited, leo imekabidhi
hundi ya Sh Milioni 423.5 kwa bodi ya ligi kuu ya
vodacom Tanzania bara kwa ajili ya haki za
matangazo ya Telesheni ya ligi hiyo.
Fedha zitagawiwa kwa klabu 14 za ligi kuu, Azam
FC, Simba SC, Yanga SC, Mtibwa Sugar, Kagera
Sugar, Ndanda FC, Polisi Morogoro, Coastal Union,
Mgambo JKT, Stand United, JKT Ruvu, Ruvu
Shooting, Mbeya City na Prisons kila kilabu ikipata
Sh. Milioni 27.5, hiyo ikiwa ni awamu ya pili ya
mgawo wa Sh. Milioni 110 za msimu.
Mtendaji mkuu wa Azam Media Limited, Rhys
Torrington amesema sehemu ya fedha
walizokabidhi hii leo ni awamu ya pili, na awamu
mbili zilizobaki zitatolewa mzunguko wa pili wa ligi
hiyo utakaoanza mwaka 2015.
“Nia ya Azam Media Limited kudhamini ligi kuu ni
kutaka iwe na ushindani ambao utaleta mvuto na
iwe nzuri zaidi miongoni mwa ligi za Afrika
Mashariki,” Amesema bosi huyo wa Azam Media.
Amesema kwa sasa Azam Media Limited imetanua
wigo wa huduma zake na inaonekana karibu nchi
zote za ukanda wa Afrika mashariki na kati, hivyo
ni imani yao ligi kuu itatangazika zaidi kimataifa.
Akizungumzia michezo ya ufunguzi ya ligi hiyo
itakayochezwa mwishoni mwa juma hili, Torrington
amesema wataonyesha michezo mitatu, ambayo ni
kati ya mabingwa watetezi, Azam FC dhidi ya Polisi
Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Dar es
Salaam, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro na Simba SC dhidi ya Coastal
Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mtendaji mkuu wa ligi kuu,
Silas Mwakibinga amewashukuru Azam Media
Limited kwa udhamini huo mzuri na kutekeleza
vizuri Mkataba wao.
Mwakibinga pia ametoa wito kwa waamuzi wa ligi
Kuu kutenda haki katika maamuzi yao ili timu bora
zishinde.
“Na pia kwa kupata fedha hizi mapema, naamini
sasa klabu hazitakuwa na visingizio wala
kelele,”amesema Mtandaji mkuu wa TPL Board.
Amesema fedha hizo zilizotolewa leo, zinafanya
kila klabu hadi sasa iwe imepata Sh. Milioni 55
baada ya kupewa fungu la sehemu ya kwanza
mwezi Juni mwaka huu.
Azam Media Limited waliingia Mkataba wa haki za
matangazo ya Televisheni ya ligi kuu mwaka jana
na shirikisho la soka tanzania (TFF) kwa pamoja
na bodi ya ligi, wakitoa Sh. Milioni 100 kwa kila
klabu, wakati mwaka huu kuna ongezeko la
asilimia 10, na kufanya dau la Milioni 110.

TUMEAMIA HUKU