Mamia ya wasichana waliotekwa na kundi la Boko Haram nchini Nigeria wanadaiwa kuonekana wakioga na kuwapikia wanamgambo wa kundi hilo.
Aidha taarifa zinaeleza wengi wa wasichana hao wanashikiliwa katika kambi tatu tofauti nje ya Nigeria.
Mmoja wa viongozi wanaohusika katika majadiliano ya kutaka wasichana hao waachiliwe huru, Dk Steven Davis alikaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akieleza hayo.
Dk Davis, ambaye ni raia wa Australia na wenzake walio katika harakati za kuwakomboa mabinti hao, waliwaona baadhi ya wasichana hao wakioga na upande mwingine walikuwa wakiwapikia watekaji ambao ni kundi la wanamgambo wa Boko Haram.
Davis alisema majadiliano ya kutaka kuachiliwa kwa wasichana hao yalikuwa katika hatua za mwisho kufanikiwa lakini makamanda wa kundi hilo walipinga wazo hilo dakika za mwisho wakihofia kukamatwa.
Hata hivyo, alisema juhudi zozote za kuwanusuru wasichana hao kwa nguvu hazitafua dafu isipokuwa kwa njia ya mazungumzo na makubaliano ya amani.
Mei 14, Serikali ya Nigeria ilieleza kuwa ipo tayari kufanya mazungumzo na kundi hilo kuwezesha kuachiwa kwa wasichana hao zaidi ya 200.
Waziri wa Elimu, Tanimu Turaki, alisema serikali ipo tayari kwa mazungumzo. Alisema kuwa waliamua hatua hiyo itumike kwa kuwa utekaji huo umeibua hali ya hofu kuhusu ulinzi wa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini humo.
Baada ya utekaji huo, Boko Haram walijinadi kuwa, watawauza mabinti hao kama watumwa. Rais Goodluck Jonathan alipitisha kuwaachia wafungwa wao lakini waziri huyo alisema imekuwa vigumu kujadiliana.
Hata hivyo, Serikali ilisema njia zote za kuwapata wasichana hao ziko mezani na wapo tayari kwa majadiliano lakini kundi hilo limekuwa likibadili uamuzi mara kwa mara.
Boko Haram ilionesha katika video inayosadikiwa kuwa ni ya wasichana hao, kundi la mabinti takribani 130 wakiwa wamevaa vazi za kiislamu la hijabu lakini hawakueleza video hiyo imechukuliwa wapi na lini.
Wasichana hao wakiwa mchanganyiko, wakristo na waislamu walitekwa na kundi hilo usiku wa Jumatatu, Aprili 14 mwaka huu katika hosteli ya shule mjini Chibok, Jimbo la Borno.