Featured Posts

Monday, June 30, 2014

MAMA WA MTOTO WA MIAKA MIWILI,ASEMA: ‘HATA MIMI NAPENDA KUISHI KAMA WENGINE’

NI kweli kama binadamu hujafa hujaumbika! Maana ya msamiati huu ni kwamba, siku binadamu anapoingia kaburini ndipo kuumbika kwake kulivyo!
Selitian Nata (25) mkazi wa Kijiji cha Kisogo Kata ya Vigwaza Wilaya ya  Bagamoyo, Pwani amejikuta katika wakati mgumu kufuatia mguu wake wa kushoto kuvimba mfano wa tende kwa ugonjwa ambao bado haujapata tiba.
Selitian Nata (25) mkazi wa Kijiji cha Kisogo Kata ya Vigwaza Wilaya ya  Bagamoyo, Pwani anayesumbuliwa na uvimbe mguuni.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo mwenye mtoto wa kike wa miaka miwili, kabla mguu huo haujafika kwenye kuvimba alianza kwa kuhisi maumivu makali sana.
TATIZO LILIVYOANZA
Anasema: “Ilikuwa mwaka 2004, kilianza kitu kama kipele baadaye uvimbe wa kawaida lakini cha ajabu uvimbe huo ukawa unanisababishia maumivu makali mno mpaka kujiuliza ni kitu gani? Sikuamini kama ni uvimbe wa kawaida.
“Kadiri siku zilivyokuwa zikienda mbele ndipo uvimbe nao ulizidi kuongezeka na kufikia usawa wa kwenye mbavu zangu. Hali hii ilinitisha sana kiasi kwamba nikaanza kukosa amani na imani ya kuishi.”
TATIZO JUU YA TATIZO
“Mbali na maumivu hayo, likazuka tatizo jingine. Nikawa napata homa kali sana hasa nyakati za usiku.
“Lakini pamoja na hali hiyo sikukaa nyumbani tu, nilijitahidi kuhangaika kwa kwenda hospitali mbalimbali ikiwemo ya Tumbi (Kibaha) lakini sikupata matibabu yoyote zaidi ya vidonge ambavyo niliambiwa ni vya kutuliza maumivu lakini uvimbe uko palepale.”
...Hivi ndivyo mguu wa kushoto wa mama huyu unavyoonekana .
ANACHOOMBA
Nata anasema: “Niko kwenye wakati mgumu kama mnavyoniona, napata shida sana. Naomba nisaidiwe. Naomba wataalamu mbalimbali pamoja na wafadhili wajitokeza niweze kupata matibabu sahihi ambayo yataondoa uvimbe huu ili na mimi niweze kuishi kwa raha kama wengine.” 
BABA WA MGONJWA
Kwa upande wake baba mzazi wa Nata aliyejitambulisha kwa jina moja la Mumbi alisema kuwa, baada  ya kugundua gonjwa hilo kwa mwanaye alimpeleka hospitalini ili akapate matibabu lakini alichokibaini huko hakuna mafanikio yoyote zaidi ya mwanaye kuendelea kuteseka kila kukicha.
ALALAMIKIA MATIBABU
Mzee Mumbi alilalamikia matibabu ambayo binti yake amekuwa akiyapata  ambapo alisema si ya kuridhisha hivyo kumfanya mwanaye asipate nafuu yoyote ile zaidi ya kuendelea kuteseka.
“Kusema ule ukweli nilimehangaika sana mahospitalini lakini hakuna cha maana. Matibabu siyo mazuri, mwanangu anaendelea kuteseka tena akiwa na mtoto mdogo kama hivyo unavyomuona.
“Lakini kupitia nyie waandishi wa habari, nawaomba wasamaria wema wamsaidie binti yangu kwa hali na mali ili aweze kupata matibabu sahihi ambayo najua ni gharama kubwa,” alisema Mumbi.
KWA NINI ALIKATA TAMAA?
Baba huyo alizidi kuweka wazi kwamba, ilifika mahali aliamua kuacha kumpeleka mwanaye hospitalini.
 Aidha, alisema kuwa anashangaa kuona kila anapokwenda hospitali mwanaye anapewa vidonge tu jambo ambalo linafanya wakate tamaa.
KUTOKA KWA MHARIRI
Uwazi linafuatilia namba ya mawasiliano ya mwanamke huyo, ikishapatikana itatoa gazetini ili walioguswa wamsadie.

TUMEAMIA HUKU