Serikali ya Sierra Leone imeonya kuwa ni hatia kumpa hifadhi mtu yeyote aliyeambukizwa virusi vya Ebola.
Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo, baadhi ya wagonjwa wa homa hiyo kali wametoroka hospitalini katika wilaya ya Kenema, kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo.
Shirika la afya duniani, WHO, limetoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa kudhibiti homa hiyo katika kanda ya Afrika Magharibi ambapo hadi sasa wagonjwa 400 wamefariki.
Mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo ndio mkubwa zaidi kushuhudiwa hasa kwa kuwa umesabaisha vifo vingi na kuenea zaidi katika nchi nyinginezo za kanda hiyo.
Visa zaidi ya 600 vya ugonjwa huo vimeripotiwa nhini Guinea ambako ulianza miezi minne iliyopita na katika mataifa jirani ya Sierra Leone na Liberia.
Takriban asilimia 60 ya watu walioambukizwa ugonjwa huo wamefariki.
Shirika la afya duniani linasema kuwa watu 46 wako katika hali mahututi kati ya 176 walioambukizwa ugonjwa huo.
Mmoja wa madaktari wanaosaidia katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo alisema kuwa baadhi ya watu wamewapuuza katika juhudi zao za kuwahamasisha umma kuhusu homa hiyo hatari.
Alisema watu wamekuwa wagumu wa kuelewa na pia hawataki kuelimishwa wakiona kama ugonjwa huo sio tisho.
WHO limetahadharisha mataifa ya Ivory Coast, Mali, Senegal na Guinea Bissau kuwa macho kutokana na wasafiri wanaoingia nchini humo kwani huenda wakawa wameambukizwa homa hiyo.
BBC