Miss Tanzania 2001 na mwanamitindo wa kimataifa Millen Magese amekumbuka kauli ya kwamba mipango si matumizi, kutokana na kuwa na mipango mingi na marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake katika kuikomboa sanaa ya filamu nchini Tanzania, lakini kabla hawajakutana naye mauti yalimkuta...
Millen na muigizaji maarufu nchini Nigeria, Ramsey Noah walipanga kukutana na Kanumba lakini kabla siku hiyo haijafika kifo kilimkuta Kanumba na mipango yote ikaharibika....
Millen |
Millen alifafanua hayo katika mahojiano maalumu wakati akitangaza kampeni yake ya kuhamasisha wanawake wanaosumbuliwa na maumivu ya tumbo yasiyo ya kawaida pindi wanapokuwa katika mzunguko wa hedhi zao ambapo kitaalam hujulikana kama Endometriosis ambapo amegundua kwamba kati ya wanawake 100 wa Tanzania, wanawake 12 hadi 15 wanasumbuliwa na tatizo hilo...
Star wa Nigeria Ramsey Nouh na marehemu Steven Kanumba |
Akikumbuka siku ya kifo cha Kanumba kabla hawajakutana na kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusiana na filamu za Tanzania na namna ya kupiga hatua nyingine mbele,Millen alisema:
"Iliniuma sana kipindi kile maana nilikuwa nipo nchini na tulipanga mimi, Kanumba na Ramsey Noah lakini ndio ikawa hivyo lakini kwa filamu zetu bado tunatakiwa kusoma zaidi ili tujue mambo mengi na pia tutengeneze wigo mpana wa marafiki kutoka nje kama mimi kwa sasa nina marafiki wengi akiwemo Ramsey Noah, Genevieve Nnaji, Albal na wengine wa Marekani"
Katika kusaidia tasnia hiyo, mrembo huyo anayemhusudu mrembo na mwanamitindo Tausi Likokola,Iman,Flaviana Matata, na Harieth Paul alisema mwelekeo wake baada ya kukamilisha masomo yake ya uigizaji, ataandaa filamu yake binafsi itakayoelezea maisha yake halisi na tatizo linalomkabili na pia ataandika hadithi kuhusiana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Albino.
"Kwa sasa nasomea namna ya kuongoza filamu katika chuo cha New York Film Academy nchini Marekani, nikimaliza nitaingia kwenye filamu na kuleta mabadiliko katika uandishi wa hadithi za filamu hizo tofauti na filamu nyingi za hapa nchini ambazo nyingi hutambua zinavyoishia baada ya kuitazama mwanzo hivyo kupoteza ladha ya kuitazama," alisema Millen na kuongeza:
Millen |
"Movies zetu za hapa Tanzania zinakosa watunzi wazuri wa hadithi maana nyingi zikianza unajua zitakapoishia,hivyo tunatakiwa tujuane na wasanii mbalimbali kutoka nchi mbalimbali kama ninavyowafahamu baadhi yao kutoka nchini Nigeria na baadhi ya wasanii wakubwa nchini Marekani ndipo filamu zetu zitafika mbali," anasema Millen.
Pia model huyo wa kimataifa chini ya Ford Models New York alifafanua sababu inayomfanya asishuke katika tasnia ya urembo akidai inatokana na kujituma kwake, kujifunza zaidi na kutoridhika na mafanikio aliyoyapata huku akiongeza kwamba anaishi na kuwaheshimu vizuri wanaomuongoza pamoja na watu wote wanaomzunguka hasa nchi yake.