Dar es Salaam.Mume wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili, anatuhumiwa kumbaka shemeji yake mdogo 17.
Taarifa za tukio hilo ziliripotiwa juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule), zikimtuhumu mwanamume huyo kwamba alimbaka binti huyo mara tatu na kumsababishia maumivu makali.
Binti huyo alifika katika kituo hicho cha polisi akiwa na ndugu zake wawili ambao walilalamika kwamba kulikuwa na jitihada kubwa kutoka upande wa mtuhumiwa wa kuzima kesi hiyo.
Akizungumza na blog hili nje ya kituo hicho, binti huyo alisema shemejiye alimbaka mara ya kwanza, Ijumaa iliyopita na Jumapili alipombaka mara mbili ndani ya gari.
Alisema mara ya kwanza alikaa kimya baada ya mtuhumiwa kumtishia kwamba angemdhuru kama angetoa taarifa ya tukio hilo alilofanyiwa wakiwa sebuleni nyumbani kwako Tabata Kimanga, lakini aliamua kutoa taarifa kwa ndugu zake baada ya kubakwa mara ya pili.
Polisi katika kituo hicho walithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo lakini walishindwa kwenda kumkamata mtuhumiwa kwa maelezo kwamba hawakuwa na askari wa kutosha na kuahidi kwamba angekamatwa jana. Hata hivyo, hadi jana mtuhumiwa huyo alikuwa hajakamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi kutwa nzima ya jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na kila simu yake ilipopigwa (kati ya saa nane mchana na saa mbili usiku), ilipokewa na msaidizi wake akisema bosi wake ana kazi nyingine.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hakuwa amepokea taarifa yoyote ya aina hiyo.
Mwimbaji anena
Alipoulizwa jana, mwimbaji huyo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani tuhuma zinazomkabili mumewe na kwamba alikuwa anajisikia vibaya kutokana na tukio hilo kuhusisha watu wake wa karibu.
“Of course (bila shaka), hili sio tukio zuri. Kwa sasa sina uwezo wa kuzungumza kwa sababu hili suala lipo Polisi. I am confused (nimechanganyikiwa), ukizingatia kwamba linasemekana kutokea wakati sikuwepo nyumbani, naomba tuzungumze baada ya akili kutulia,” alisema.
Kadhalika, jana saa 6:20 mchana, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mtuhumiwa ambaye baada ya kupewa maelezo kuhusu tuhuma zinazomkabili alisema: “Samahani sana ujue sikusikii kabisa,” kisha alikata simu.