Kelele, kukunjana na kunyoosheana vidole jana mchana vilitawala nje ya ukumbi wa Bunge wakati wabunge wa CUF kutoka Zanzibar walipotaka ‘kumkanya’ Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.
Sakata hilo la aina yake lililodumu kwa takriban dakika 15 lilitokea saa 7:05 mchana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge.
Wabunge hao Mussa Haji Kombo (Chakechake), Kombo Khamis Kombo (Magogoni) na Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), walitaka ‘kumkanya’ Keissy kutokana na kile alichosema alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2014/15 na kusema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.
Kauli hiyo licha ya kulalamikiwa na wabunge wote wa CUF kutoka Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kusimama na kuomba mwongozo wa Spika, Keissy alizidi kuwashambulia na kusema kuwa majimbo ya Zanzibar watu wake wanaweza kukusanywa sehemu moja kwa kupigiwa filimbi tu.
“Nyie Zanzibar idadi yenu ya watu ni asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania. Sasa mnataka kupata kila kitu sawa ili iweje! Mnataka ajira asilimia 21 na Watanganyika wakafanye kazi wapi?” alisema Keissy.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho na wabunge kuanza kutoka nje, wabunge hao wa CUF walikwenda kumsubiri Keissy karibu na jengo la kantini.
Mbunge wa kwanza kumvaa Keissy alikuwa Khamis Kombo ambaye kabla ya kumfikia alizuiwa na Mbunge wa Mpanda Kaskazini (CCM), Moshi Selemani Kakoso.
Wakati Keissy akishangaa alitokea Haji Kombo ambaye naye alizuiwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Abdulsalaam Selemani Amer.
“Mimi sitaki kupigana bwana ninachokijua ni kwamba nilikuwa nikichangia mjadala wa bajeti na nilichokisema ni ukweli mtupu,” alisema Keissy huku akiwa amenyanyua mikono yake juu na kuondoka eneo hilo.
“Wewe (Keissy) sijui una nini wewe. Unapenda kutufuata fuata sana watu wa Zanzibar. Hivi una nini wewe? Hivi hujui kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar?” alisikika akisema Khamis Kombo.
Kwa upande wake, Sanya hata baada ya wenzake kutawanyika eneo hilo, aliendelea kumlaumu Keissy na kuwataka wabunge wa CCM kumuonya.
“Anapenda sana kutoa kauli mbaya dhidi ya Zanzibar. Jamani mkanyeni mwenzenu haiwezekani kila siku awe yeye tu anayetukashifu bungeni,” alisema Sanya huku akitulizwa na mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Jabiri Marombwa.