Suala la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata limechukua sura mpya baada ya mzazi mwenza wa mchumba wa mbunge huyo, kukanusha taarifa kwamba alikwenda Dodoma kwa lengo la kuomba msaada kwa viongozi wa Bunge.
Kauli ya mama huyo imezidisha utata katika sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa hiyo iliyokuwa ifanyike Jumamosi baada ya kutokea habari kuwa mwanamke mmoja alikwenda bungeni mjini Dodoma kutaka kuonana na Spika kwa lengo la kuomba Bunge limsaidie kupata haki yake kabla ya harusi hiyo kufungwa na hivyo kusababisha harusi kutofanyika.
Kamata, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na wimbo wake wa “Wanawake na Maendeleo” na baadaye kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, alikuwa afunge ndoa na mtu aitwaye Charles Gardiner Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini haikufanyika kutokana na mbunge huyo kuwa mgonjwa kiasi cha kulazwa hospitali maeneo ya Tabata.
Jana, Kinavi Dadi, ambaye ni mzazi mwenza wa Gardiner, alikanusha kufunga safari hadi Dodoma kwa lengo hilo.
“Ni kweli kwamba Charles ni baba watoto wangu, lakini sijawahi kwenda Dodoma na wala sifahamu chochote kuhusu safari hiyo. Nadhani inatosha,” alisema mama huyo na hakutaka mazungumzo zaidi.
Baadaye kidogo mmoja wa ndugu wa Kinavi, ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini, alikiri ndugu yao kufunga ndoa na Gardiner Juni 2004 na kujaliwa kupata watoto wawili, lakini walitofautiana na baadaye ndoa yao kuvunjwa mwaka 2012.
“Ni kweli kwamba dada yetu alifunga ndoa na Charles, lakini pia ni kweli kwamba walipeana talaka halali two years ago (miaka miwili iliyopita), kwa hiyo taarifa kwamba eti amezuia ndoa isifungwe, siyo za kweli na wala huko Dodoma hajawahi kwenda,” alisema.
Alisema taarifa kwamba aliyepata kuwa mke wa Gardiner alikwenda Dodoma kuomba msaada wa Bunge zimewaumiza sana kama familia kutokana ukweli kwamba Kinavi ndiye anayefahamika kuwa mke wa kwanza.
“Ndugu yetu analia sana kutokana na kuumizwa na wale wanaomchafua. Sisi katika familia tumelelewa kwa maadili hivyo Kinavi siyo mtu wa kuzuia ndoa ya Gardiner maana walishatengana, mawasiliano yaliyopo ni yale yanayohusu watoto ambao wana haki ya wazazi wote wawili. Hatujui waliozitangaza hizo habari walikuwa na malengo gani,” alisisitiza.
Bungeni Dodoma
Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka bungeni Dodoma zinasema mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa Gardiner ni ‘feki’ na alikuwa wa kutengenezwa na baadhi ya wabunge kwa lengo la kumtibulia Kamata.
Mpango huo unadaiwa kuwahusisha wabunge wanawake wanne; watatu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka Chadema ambao awali waliapa kwamba ndoa ya mbunge mwenzao isingefungwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandishi wa Mwananchi waliopo Dodoma walimsaka mwanamama huyo bila mafanikio na baadaye waliambiwa kwamba haikuwa rahisi kumwona kwani hakuwa halisi.
Kundi la wabunge hao ndilo lilimwingiza mwanamke huyo katika viwanja vya Bunge kwa lengo la kumkutanisha na viongozi wa taasisi hiyo, lakini mpango huo ulishindikana.
Mwishoni mwa wiki, Naibu Spika Job Ndugai alisema anakumbuka kwamba alipewa taarifa za kuwapo kwa mwanamke anayemtafuta, lakini hadi alipoondoka kwenda jimboni kwake Kongwa hakuwa ameonana naye.
“Walioniambia ni wabunge fulani na walikuwa kama wanafanya utani, lakini hadi naondoka kuja huku Kongwa, maana niko vijijini kwa sasa, sikubahatika kuonana naye kwa hiyo simfahamu kwa jina, wala sura yake, wala anakotoka sikufahamu,”alisema Ndugai.
Juzi Kamata aliliambia gazeti hili kwamba naye alisikia taarifa za kuwapo kwa mwanamke huyo mjini Dodoma, lakini hakuweza kufahamu ni nani kutokana na kwamba alikuwa bado amelazwa hospitalini.
Mbunge huyo alilazwa kwa siku sita katika Hospitali ya Tabata General, iliyopo Segerea, Dar es Salaam na aliruhusiwa juzi. Anatarajia kwenda Dodoma wakati wowote.
Mapenzi ya Mungu
Mbunge huyo juzi alizungumzia kutofungwa kwa ndoa yake na kusema anaamini kilichotokea “ni mapenzi ya Mungu”.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Sinza jijini Dar es Salaam, Kamata alisema ingawa ndoa hiyo haijafungwa, moyo wake una amani kwa kuwa alimwomba Mungu kuhusu suala hilo kwa muda mrefu na hicho ndicho Mungu alichojibu.
“Hii ni mipango ya Mungu. Wakati wa maandalizi ya ndoa tulikuwa na timu ya wanamaombi. Tuliomba sana na baada ya kuiombea ndoa, tuliomba mapenzi yake yatimizwe. Kwa hiyo haya ni mapenzi yake,” alisema.
Kamata alisema licha ya kuwa tukio la kutokufungwa kwa ndoa hiyo kuwa zito na ambalo lingeweza kumjeruhi moyo, amekuwa na amani tofauti na ndugu, jamaa na marafiki zake wengi walivyodhani.
“Mimi mwenyewe nilikuwa najishangaa, mbona nina amani. Nashangaa tarehe 24 inapita hivi hivi, na ikathibitika ndoa haijafungwa, lakini bado nina amani,” alisema.
Aliongeza kuwa anaamini kutokufungwa kwa ndoa yake kuna sababu ambazo Mungu mwenyewe anazijua na wala hawezi kumlaumu mtu au kulaani chochote kilichoingilia kati kufungwa kwa ndoa hiyo.
“Naamini ni mipango ya Mungu, yeye ana makusudi yake. Huwezi kujua ndoa ingefungwa nini kingetokea, lakini nina amani moyoni na maisha yanasonga mbele,” alisema.
Kuhusu maandalizi ya harusi, alisema mipango mingi ilishafanyika na baadhi ya fedha zililipwa, lakini majadiliano yanafanyika kama waliokwishalipwa wanaweza kurudisha angalau nusu ya fedha.
Alisema baadhi ya fedha zilishalipwa kwa mpambaji, mpishi na mavazi ya harusi lakini ukumbi na vinywaji havikuwa vimelipiwa.
chanzo:mwananchi