WAKATI waumini wa makanisa mbalimbali wamekuwa wakiamini kuwa wachungaji ni watu wenye uwezo wa kuwaondolea matatizo yao, yakiwemo magonjwa, Mchungaji Langeni Mwasibira (39) wa Kanisa la Baptist, lililopo Kyela mkoani Mbeya yupo hoi hospitalini Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mchungaji huyo yupo katika mateso makubwa baada ya gonjwa la ajabu kumkumba na kuwapa hofu waumini wake, ambao hata baada ya kufunga kwa ajili ya maombi, hali yake inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
Mwasibira, mkazi wa Kijiji cha Kisyosyo Kata ya Matema yupo Muhimbili, Jengo la Sewahaji, wodi namba 23 akijiuguza baada ya kulazwa katika hospitali mbalimbali nchini bila mafanikio.
Akisimulia kwa uchungu kisa cha ugonjwa wake huo, alisema ulimuanza mwaka 1994, tena ukiwa kama kijidoa cheusi kabla ya kugeuka kipele ambacho alipokwenda hospitali ya wilaya yao ya Kyela kwa ajili ya kupimwa na kutibiwa, madaktari walishindwa kugundua tatizo na kumshauri kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
“Hiyo ilikuwa imeshachukua miaka minne sasa, hivyo mwaka 1998 nikaenda Mbeya, lakini nako walishindwa kuniambia tatizo langu hasa lilikuwa ni nini, uvimbe, muwasho na maumivu makali yalikuwa yanaongezeka, ikawalazimu kunifanyia upasuaji, lakini hakukuwa na unafuu zaidi ya uvimbe kuzidi kuumuka na maumivu kuongezeka,” alisema.
“Nikawa sipati usingizi kutokana na maumivu, mwaka 2000 nilifunga safari ya kuja Muhimbili, nao walinipeleka hospitali ya magonjwa ya kansa Ocean Road, nilipimwa lakini haikua kansa, nilirudishwa tena Muhimbili, walinipima kwa mara nyingine wakagundua kuwa ni ugonjwa wa neurofibroma, walidai wakiupasua utaumuka zaidi hivyo nirudi nyumbani.
“Nililazimika kurudi nyumbani Mbeya, hata hivyo hali ilizidi kuwa mbaya, wakati mmoja nikasikia Kigoma kuna daktari bingwa wa magonjwa haya, nikalazimika kufunga safari, nako walifanya upasuaji, matokea yakawa mabaya zaidi, ulizidi kuvimba kiasi cha kukaribia kufunika jicho.
“Nikiwa huko niliishiwa fedha, nililazimika kupiga simu nyumbani ambako walifanya mchango wa hela kwa ajili ya nauli yangu nirudi nyumbani, hata hivyo hali ilikuwa mbaya, nikaona bora nije tena hapa Muhimbili Aprili 21, mwaka huu.
Alisema anawashukuru madaktari kwani walimpokea kwa upendo na kumchukua vipimo kwa mara nyingine, ambavyo hata hivyo, bado havijatoka.
Wakati yeye akiwa hoi kitandani Muhimbili, maumivu mengine yaliongezeka hivi karibuni, baada ya kupokea simu kutoka kwa ndugu zake, ikimfahamisha kuhusu kusimamishwa shule kwa watoto na mdogo wake ambao alikuwa akiwasomesha kutokana na kutolipwa kwa karo wshilingi laki tisa.
“Nina mke na watoto watano, kwa sasa mke wangu ndiye anahangaika nao,” alisema.
Kwa walioguswa na habari hii wawasiliane naye kwa namba zake ambazo ni 0758 902 884 au 0786 557 612.