Singida. Dereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Juma Juma (52), amefariki dunia wakati akifanya mapenzi kwenye nyumba ya kulala wageni akiwa na mwanamke ambaye imedaiwa ni mhudumu wa baa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo lilitokea Mei 3, saa 4:00 usiku chumba kwenye Na. S.2 cha nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Top Life New mjini Kiomboi.
Alisema saa 6:00 usiku siku ya tukio hilo, dereva huyo alimuaga mpangaji wake kuwa anatoka mara moja na hangechelewa kurudi nyumbani kwa hiyo asifunge mlango wa mbele ya nyumba.
Alisema kuwa saa mbili baadaye, dereva huyo alionekana akiwa baa iliyoko kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni ambayo iko mita 50 kutoka nyumbani kwake.
“Muda huo Juma alionekana akiwa na mmoja wa wahudumu wa baa hiyo aitwaye Agness Mayo (32) anayesadikiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi,” alisema.
Kamwela alisema mhudumu huyo wa baa alitoweka Mei 4, mwaka huu baada ya kuaga kwamba anakwenda kanisani na kutorokea kusikojulika.
Hata hivyo, ufunguo wa chumba alicholala Juma zilikutwa chumba cha kulala wahudumu wenzake.
Kamanda huyo alisema kuwa tangu siku Mei 3, chumba alicholala Juma hakikufunguliwa hadi Mei 5 mwaka huu wakati mwili wa dereva huyo ulipokutwa ukiwa umeharibika.
“Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kutafuta mhudumu aliyetoroka ili ahojiwe na kisha kufikishwa mahakamani endapo atabainika kuhusika na tukio,” alisema kamanda Kamwela.