JESHI la Polisi mkoani Geita, linamshikilia William Kibyala (40), mkazi wa Kijiji cha Misiri, Kata ya Bugarama, Wilayani Geita kwa kosa la kumpaka pilipili machoni mwanae John Wiliam (4), na kumchapa viboka sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Joseph Konyo, amethibitisha Jeshi hilo kumshikilia mtuhumiwa huyo muda mfupi baada ya tukio hilo lililotokea Mei 23, 2014 ambapo amesema mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
“Mtoto huyu alifariki baada ya kupewa adhabu na Baba yake mzazi kwa kupigwa na kupakwa pilipili, huyu mtuhumiwa tunamshikilia hadi sasa na uchunguzi zaidi wa tukio hili bado unaendelea kwahiyo kwa taarifa nyingine tutawaambia ili muujulishe Umma wa watanzania kupitia kwenu na vyombo vingine vya habari” alikaririwa Konyo katika mahojiano na mwandishi wetu
Aidha, alisema Baba wa mtoto huyo anadaiwa kufanya ukatili huo baada ya kumtuhumu mtoto huyo kukataa kumfungulia mlango wakati alipotoka matembezini usiku wa manane.
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Kijiji hicho wamedai kuwa mtoto huyo alifariki baada ya kuchapwa fimbo mwili mzima, kupigwa ngumi na mateke, kisha kupewa adhabu ya kukimbia riadha ya kuzunguka nyumba yao usiku wa manane kabla ya kifo chake.
Mmoja wa mashuhuda hao, Irine Kaijage, amesema baada ya mtoto huyo kumaliza adhabu hiyo alipakwa pilipili machoni na makalioni hali iliyosababisha mtoto huyo kuzidiwa na kupoteza maisha Mei 24, 2014 jioni.
Mmoja wa watoto wa Mzazi huyo, Shija William, alisema mdogo wao alikuwa akipewa adhabu hiyo mara kwa mara na Baba yao kwa madai kwamba Mama yao alimbambikizia mdogo wao kwani yeye hakumzaa.