WATOTO watatu wa familia moja, wakazi
wa Nyankumbu, Wilaya ya Geita, mkoani
Geita, wamefariki dunia usiku wa
kuamkia jana baada ya nyumba yao
kuteketezwa kwa moto uliowashwa kwa
mafuta ya petroli na mtu asiyefahamika.
Dada mkubwa wa marehemu hao ambaye
ni mwanafunzi wa kidato cha pili
Sekondari Mwatulole na wazazi wao,
walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo
ambalo chanzo chake ni ugomvi wa ardhi.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya
hiyo, Dkt. Adam Sijaona, alisema miili ya
watoto hao imehifadhiwa hospitalini
hapo.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni
Reginald Robert (9), mwanafunzi wa
darasa la nne Shule ya Msingi Nyankumbu
Mkombozi, Sophia Robert (6) aliyekuwa
akisoma darasa la kwanza shuleni hapo
na Remijius Robert (4).
Majeruhi ni Scholastica Robert (15),
ambaye amejeruhiwa vibaya sehemu
mbalimbali za mwili wake ambapo hivi
sasa anaendelea na matibabu katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Wazazi wa watoto hao ambao pia
walijeruhiwa katika tukio hilo ni Bi.
Angelina Gaspa (36), ambaye amelazwa
hospitalini hapo akiwa na majeraha
katika mkono wake wa kulia, mgongoni,
begani pamoja na Bw.Robert Remijius (45)
aliyejeruhiwa kichwani.
Akizungumza kwa tabu akiwa wodini, Bi.
Gaspa alisema siku ya tukio walikuwa
wamelala watoto wakiwa chumbani kwao
ambapo ghafla alisikia watoto wakipiga
kelele na kusema ‘mama tunakufa’ na
alipokwenda kuwaangalia, akakuta
nyumba inateketea kwa moto.
“Nilikuta nyumba nzima ikiwaka moto,
tulipiga kelele za kuomba msaada kutoka
kwa majirani ambao walifika na kuanza
kuvunja milango pamoja na ukuta ili
waweze kutuokoa.
“Mimi na mume wangu tulijitahidi kuvunja
tofali japo tupate sehemu ya kupita na
majirani walipofanikiwa kuvunja nyumba,
tayari watoto wangu watatu walikuwa
wameteketea kwa moto,” alisema.
Aliongeza kuwa, anaamini chanzo cha
tukio hilo ni ugomvi wa ardhi uliokuwepo
kati yao na mkazi mmoja wa eneo hilo
(jina limehifadhiwa) ambaye alifika na
kuchimba kisima katika eneo ambalo wao
walilinunua kisheria lakini alidai ni lake.
“Tunaishi vizuri na majirani zetu, yote
tunamuachia Mungu kwani hata tulipotaka
kumlipa ili aondoke katika eneo letu
alikataa na mgogoro huu umedumu kwa
mwaka mmoja,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo,
Bw. Manzie Mangochie, alisema kitendo
hicho cha kikatili hakitavumilika na
aliyefanya tukio hilo lazima asakwe kwa
nguvu zote ili aweze kufikishwa katika
vyombo vya sheria mara moja.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kalangalala,
Bw. Hamad Hussein, alisema watu
waliofanya ukatili huo walitumia mafuta
ya petroli kuyamwaga mlangoni mwa
nyumba hiyo na kusambaa vyumbani
ukianzi katika chumba walicholala watoto
hao.
“Katika eneo la tukio, tumekuta ndoo ya
plastiki yenye ujazo wa lita tano
iliyotumika kuhifadhia mafuta hayo,
tunaomba ushirikiano kwa wananchi ili
tuwatie mbaroni wote waliohusika,”
alisema