Featured Posts

Thursday, May 8, 2014

SERIKALI YADAIWA KUFANYA SIRI UGONJWA WA DENGU

Ugonjwa wa homa ya dengue ambao umezidi kusambaa mkoani Dar es Salaam na kuathiri wilaya zake tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni umezua hofu na taharuki kubwa kwa wananchi. Takwimu za Kitengo cha Utafiti wa Magonjwa cha Ifakara (IHI), kimeweka kambi katika Hospitali ya Mwananyamala hapa jijini kutafiti aina za homa zinaonyesha kuwa, kwa miezi miwili ya Machi na Aprili pekee, wagonjwa 85 walibainika kuwa na ugonjwa huo.
Kwa siku tatu mfululizo kuanzia juzi, gazeti hili limekuwa likichapisha habari za kusambaa kwa ugonjwa huo, ambao madaktari mabingwa wa ugonjwa huo wamesema hali ni mbaya kuliko inavyodhaniwa kwa kuwa asilimia 50 ya watu wanaopimwa na kubainika kuwa na ugonjwa huo ni watu wazima kuanzia miaka 18.
Katika kuthibitisha kwamba ugonjwa huo haubagui au kuweka matabaka, madaktari watatu na muuguzi mmoja wameripotiwa kuugua ugonjwa huo, kama ilivyo kwa mmoja wa wanamuziki maarufu hapa nchini ambaye hadi juzi alikuwa amelazwa katika hospitali moja hapa jijini baada ya kuugua ugonjwa huo. Tunaambiwa kwamba hivi sasa kuna hali ya hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo na kwamba sasa mbu ni hatari kuliko ilivyokuwa awali, kwani hawa wanaoambukiza homa ya dengue ambayo haina chanjo wala tiba wanaambukiza wakati wa mchana.
Hatuoni ajabu hali hiyo inapoleta hofu na taharuki kwa wananchi, hasa pale mamlaka husika zinapothibitisha kwamba hapa jijini kuna wagonjwa wapya 20 kila siku na kwamba asilimia 2.5 ya wagonjwa huwa katika hali mbaya. Moja ya mambo yanayozidisha hofu ni kwamba mgonjwa anapobainika kuambukizwa dengue hana tiba rasmi, isipokuwa kinachotibiwa ni dalili tu. Taarifa kwamba kuna uhaba mkubwa wa vifaa na vitendanishi pia hazileti matumaini kwa wananchi, ingawa mamlaka hizo zimesema kuna wataalamu wa kutosha wanaoweza kubaini ugonjwa huo.
Kinachotatanisha zaidi ni dalili za ugonjwa huo ambazo siyo tofauti na zile za malaria. Je, kuumwa kichwa na kusikia uchovu na maumivu ya viungo siyo dalili zilezile kama za malaria? Je, ugonjwa huo kujitokeza kati ya siku tatu na 14 baada ya kuambukizwa siyo dalili za ugonjwa huo? Tofauti kati ya ugonjwa huo na malaria ni kwamba mgonjwa wa dengue hutoka damu sehemu mbalimbali za mwili kutokana na kuharibika kwa chembehai nyeupe za damu. Vinginevyo magonjwa hayo ni kama pacha wanaofanana na ndiyo sababu tunasema zinahitajika taarifa za kutosha ili wananchi wajue la kufanya pindi wanapougua magonjwa hayo.
Sisi tunadhani Serikali inastahili lawama kwa kutochukua hatua stahiki mapema kupambana na ugonjwa huo, ambao uliingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kuua wanafunzi kadhaa wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Juni mwaka jana, Wizara ya Afya ilithibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo na Machi 26 mwaka huu, ilitoa taarifa kwa umma, ikisema wagonjwa 70 walikuwa wamebainika, 58 kati yao wakiwa Kinondoni, saba Temeke na watano Ilala.
Hata hivyo, wizara hiyo haikupaswa kuishia katika kutoa taarifa tu pasipo kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi nchi nzima kuhusu ugonjwa huo, namna ya kujikinga na nini cha kufanya iwapo wataambukizwa. Ulihitajika uwazi badala ya usiri, vinginevyo ugonjwa huo usingeenea kwa kasi tunayoishuhudia hivi sasa.

TUMEAMIA HUKU