Featured Posts

Friday, July 25, 2014

JE WAJUA HII? MWIMBWJI WA INJILI UPENDO NKONE, ANUSURIKA KULAANIWA

Makala: Gabriel Ng’osha
UKISIKILIZA wimbo wake wa Hapa Nilipo, Usinipite Bwana, Usifurahi Juu Yangu na Upendo wa Yesu, hakika utagundua kwamba kuna kitu Mungu amekiweka katika ubongo wa mwimba  wa nyimbo za Injili mahiri nchini, Upendo Nkone.

Mwimbaji mahiri wa nyimbo za Injili nchini, Upendo Nkone.
Ana sauti nzuri, nyimbo zake zinagusa wengi kutokana na ujumbe mzito ambao Mungu amemtumia ahubiri Injili kwa watu wote, kila mmoja kwa nafasi yake anaguswa kumsikiliza.
Exclusive Interview imezungumza naye mambo mengi kuanzia maisha yake ya utotoni hadi alipofikia hatua ya kuwa mwimbaji mkubwa wa muziki wa Injili nchini kwa mtindo wa maswali na majibu kama ifuatavyo:
Mwandishi: Wasomaji wetu wangependa kujua historia yako japo kwa kifupi.
Upendo: Mimi ni mzaliwa wa Kijiji cha Bitale mkoani Kigoma, ni mtoto pekee wa kike na wa kwanza kati ya watoto saba, ni mkristo, nimekua na kulelewa katika maisha ya dini, babu yangu mzee Nkone akiwa ni Askofu wa Kanisa la Pentekoste (PFTC).
Ni mama mwenye watoto 6, wawili wakiwa wangu wa kuzaa, wanne wa mume wangu mpendwa aliyenioa baada ya kufariki mume wangu wa kwanza na yeye kufiwa na mkewe.
Nimemaliza masomo ya msingi na sekondari ingawa sikufanya vizuri lakini baadaye nilijiunga na chuo cha ufundi wa ushonaji cha FDC kilichopo mkoa wa Pwani, baada ya hapo maisha yaliendelea kusonga kama kawaida, nikafanikiwa kupata mume.
Mwandishi: Kitu gani unakikumbuka wakati ulipokuwa shuleni?
Upendo: Nilikuwa na tabia ya udokozi, nilikuwa naiba fedha nyumbani naenda kula maandazi shuleni wakati huo nilikuwa niko darasa la nne.
Mwandishi: Nani alikufundisha udokozi au ni tabia yako ya asili?
Upendo: Hapana kuna mmoja wa ndugu zangu ambaye alikuwa ananizidi umri ndiye alikuwa ananituma, baadaye tunagawana na kusema eti tumeokota, mchezo huo uliendelea kwa muda mrefu sana, kila wakiacha fedha nyumbani mimi nazipitia.
Mwandishi: Ukiachana na tukio hilo, unaweza kutupa tukio lingine unalolikumbuka la udokozi?
Upendo: Kuna siku ambayo siwezi kuisahau, niliiba fedha ya sadaka (fungu la kumi) ambayo bibi alikuwa katunza chini ya godoro lake kwa ajili ya kupeleka kanisani,
ila wakati naichukua ile bahasha nilikuwa na mashaka kwa namna fedha  zilivyokuwa zimewekwa kiasi kwamba hata wewe ungejua zimewekwa kwa kazi maalumu, ila kwa kichwa ngumu nikachukua tu.
Mwandishi: Haukushtukiwa?
Upendo: Bibi alikuwa ananipenda sana, mbaya zaidi badala ya kunihisi, aliniita na kunishitakia kuwa kaibiwa fedha yake ya sadaka na kunieleza kwamba inamuuma sana kwa sababu alipanga akamtolee bwana fungu la kumi. Ilikuwa ngumu kujitangaza ama kumrudishia moja kwa moja kwa sababu ningepigwa na ingekuwa ni aibu kwangu lakini pia mimi ndiye niliyekuwa mjukuu wake kipenzi, ningemuumiza sana.
Mwandishi: Kwani ni zilikuwa shilingi ngapi ulizokwapua?
Upendo: Kama elfu kumi kwa kipindi hicho ilikuwa na thamani kubwa kuliko sasa, bibi alikuwa anafanya biashara zake ndogondogo za kuuza mikate na mkaa tena mimi ndiye nilikuwa muuuzaji mkuu, utoto jamani! (anacheka na kusikitika kidogo).
Mwandishi: Bibi alichukua hatua gani sasa kwa kuibiwa fedha hiyo?
Upendo: Alitangaza sana kwa mtu aliyeichukua airudishe bahasha yake kwani aliweka sadaka kwa ajili ya kupeleka kanisani, baada ya kuona kimya alitangaza kutoa laana kwa aliyechukua kwa kuiba lakini kama aliiokota hatapatwa ila ni vizuri kuirejesha.
Nikaingiwa na huruma, nikamwambia twenda nikamsaidie kuitafuta, tukaingia ndani na kuanza kuitafuta baadaye nikamwambia aangalie upande wa pili wa kitanda alipoinama nikaiweka upande mwingine nikajifanya natafuta kisha nikamwambia bibi hii hapa, akaja akaichukua ila alishangaa, hivyo ndivyo nilivyofanya.
Je, Upendo Nkone alikwepaje hiyo laana mpaka sasa anaendelea kuimba na kupeta katika kumtukuza Mungu muumba mbingu na nchi? Fuatilia Jumamosi ijayo.

TUMEAMIA HUKU