SEHEMU YA KWANZA.
Mungu
ameujaalia mkoa huu kwa kuwa na milima kila sehemu na miti yenye majani
ya rangi ya kijani kibichi. Ameupa ardhi yenye rutuba iliyoweza
kuzalisha mazao mbali mbali, pia amewapa mito japokuwa kasoro yao ni
moja kubwa na ndio jina livumalo hususani ukiitaja kasoro hiyo.
Nauzungumzia
mji kasoro bahari. Si mwengine na mji wa Morogoro. Huko aliishi mzee
kambi na mtoto wake wa pekee Aisha. Hiyo ni kutokana na kumpoteza mke
wake na kuamua kuishi hivyo huku akiridhika kumlea mtoto wake huyo wa
kike aliyeachwa na mama yake akiwa na umri wa miaka sita tu.
Maisha
sio mazuri kwa upande wa kipato, ila furaha ya familia hiyo ilizika
mapengo yote ya umasikini walionao. Aisha alikua kwa kasi na kupelekwa
shule na baba yake alipofikisha umri wa miaka saba.
Kichwa
cha msichana huyo kiliwafurahisha sana walimu wake kutokana na uwezo wa
darasani aliokuwa nao. Alishika nafasi ya kwanza kuanzia darasa la
kwanza hadi darasa la sita ambapo aliachishwa shule na baba yake mkubwa
baada ya baba yake mzazi kupooza viungo kuanzia kiunoni kushuka chini.
Walimu
na wanafunzi wenzake walisikitishwa na hatua hiyo, lakini hawakuwa na
la kuamua japokuwa waliamini kuwa angemaliza darasa la saba, basi lazima
angefaulu tena kwa kiwango kikubwa.
Kazi
ya kumuhudumuia baba yake aliachiwa peke yake. Hadi kuna vitu vingine
kama kumsafisha pindi baba yake alipojisaidia aliifanya yeye mtoto wa
kike huku ndugu zake wakiwa wanakuja kwa nadra sana kuwatembelea.
Mzee
kambi alikua analia kila siku na kumuomba mungu amchukue ili mtoto wake
asipate yale mateso aliyokuwa anayapata juu yake. Siku moja Shani
alitumwa na baba yake aende akamtafutie ndulele kwa kua alikuwa anashida
nazo.
Kwakua
walikua wanaishi mbali kidogo na shamba lao, ilimchukua dakika ishirini
kwenda na kurudi baadae baada ya dakika zipatazo arobaini na tano toka
alipotoka pale.
“baba…babaaaaaaaaaaaaa’
Alilia kwa uchungu Aisha baada ya kumuona baba yake amekata roho baada
ya kujichoma na kisu alichokua anakitumia kummenyea baba yake machungwa.
Kilio
kilikua zaidi na majirani walikisikia kilio kile na kukusanyika eneo la
tukio. Waliungana na yule mtoto na wengine wakimpooza mazito yaliyo
mkuta. Baada ya mazishi ya mzee Kambi, baba mkubwa wa Aisha alichukua
jukumu la kumlea mtoto huyo.
Ukurasa
mpya wa mateso kutoka kwa mama yake mkubwa na baba yake huyo
ulifunguliwa baada tu ya arobaini ya mzee kambi. Aligeuzwa mfanyakazi wa
ndani kwenye nyumba ya marehemu wazazi wake, alichota maji, kufua nguo
za watu wote mule ndani na kila kazi zenye uhusiano na ile familia, basi
alizifanya yeye.
Maisha
ya tabu,dhiki,mateso na msoto ndio uliomkuza Aisha. Ugumu wa maisha na
kutafutiwa wanaume kwa ajili ya kuolewa kinguvu ndio vitu vilivyomchosha
Aisha na kuamua kutoroka nyumbani kwao na kukimbilia kijiji cha pili.
Huko
alipata hifadhi na mama mmoja baada ya kumuhadithia kila kitu
kilichohusu maisha yake. Kwa imani ya yule mama, alimkaribisha na kuanza
kuishi naye kama mtoto wake. Uzuri uliofunikwa na shida miaka mingi
iliyopita, ulianza kuonekana taratibu kama kijua cha asubuhi
kichomozapo.
Hali
iliyofanya vidume vya kijiji hicho kumtolea macho. Alinawiri vizuri
kutokana na matunzo ya yule mama ambaye alifaidika naye kutokana na yeye
alivyokuwa anajituma. Aisha alipotimiza miaka ishirini na moja,
alifanikiwa kumpata ampendaye pale kijijini.
Alianzisha
uhusiano na mvulana huyo wa kwanza katika maisha yake kwa makubaliano
ya kutofanya mapenzi mpaka ndoa. Kutokana na uelewa na mapenzi ya dhati
aliyokuwa nayo ZAKARIA, alikubaliana na Aisha na mapenzi yao yalinoga
bila kushiriki kitendo hicho. Kila mahali walikuwa wote na walipendezana
kwa hali yao.
Hakika
walikuwa wakivutia kwa kila mahali wapitapo. Baada ya mwaka mmoja toka
waanzishe uhusiano wa kimapenzi, Zakaria aliitwa na kaka yake Dar-
es-salaam kwa ajili ya kufanya kazi kutokana na kupata nafasi aliyokuwa
anamuahidi kila siku.
Kwa
majonzi makubwa, Zakaria alimuambia kua anaenda kutafuta maisha na
yakikaa sawa basi atakuja kumchukua. Wote walilia sana na kupeana ahadi
ya kuishi pamoja tena kivyovyote vile. Zakaria aliondoka na kumuacha
Aisha peke yake.
Baada
ya miezi sita kupita, mama mlezi wa Aisha aligongwa na nyoka alipokuwa
Shambani na kupoteza maisha. Lilikua ni zaidi ya pigo kwa Aisha ambaye
hakuwa na mtegemezi mwingine pale kijijini zaidi ya yule mama peke yake.
Alilia
sana na baadae uamuzi wa kwenda kumtafuta mpenzi wake mjini
Dar-es-salaam ulimjia. Hela za pole alizozipata ndizo alizozitumia
kwenda nazo Dar, bila kujua ni wapi afikiapo, atakapolala wala chakula
atakachokula kwa siku zote atakazokuwa mjini. Yote hayo hakuyawaza zaidi
ya kuamini kuwa akifika huko ataonana na mwanaume wa ndoto zake.
ZAKARIA.