Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Askari Magereza wa kike aliyejeruhiwa kwa risasi baada ya basi la jeshi hilo kushambuliwa kwa risasi na majambazi, amesema hakuhisi mpenyo wa risasi katika titi lake la kushoto mpaka alipokaguliwa na askari mwenzake.
Askari huyo ni mmoja wa majeruhi ambao walishambuliwa kwa risasi kwenye basi la Jeshi la Magereza lililokuwa limebeba mahabusu, Julai 2, mwaka huu, baada ya kupora fedha kwenye gari lingine lililokuwa kwenye foleni, eneo la Msasani kwa Mwalimu Nyerere karibu na Hoteli ya Regency.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa taabu, Koplo Doto Sanga aliyelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili wodi namba 12 Kibasila, anasema ilichukua muda kuhisi maumivu ya risasi hiyo, kwani iliambatana na vioo wakati majambazi hao wanne waliposhambulia kioo cha mbele cha basi hilo.
“Ninachokumbuka siku hiyo tulikuwa tumetoka Kawe tunaelekea mahakama ya Kinondoni nikiwa na mahabusu wa kike, saa 8:30 mchana baada ya kufika maeneo ya Mikocheni tulikutana na foleni kwa kuwa tulikuwa tunawahisha mahabusu, dereva ‘alitanua’ (kupita pembezoni mwa barabara kukwepa foleni),” anasema Koplo Sanga na kuongeza:
“Ghafla tukaona uporaji ukifanyika mbele ambako tulikuwa tunaelekea, baada ya majambazi wale kutuona wakaona sisi tayari ni kikwazo kwao hapohapo nikawasihi mahabusu wote walale chini, wakatokea watu wawili na kushambulia basi tulilopanda kwa risasi mbele na nyuma, baada ya kuanza kwa zoezi hilo mimi, dereva na askari mwingine tukalala chini pia,” anasema.
Koplo huyo aliyelitumikia jeshi la magereza kwa miaka 14 sasa, anasema risasi ziliendelea kurindima kwa dakika chache na baadaye majambazi hao walikimbia.
“Haikuchukua muda mrefu, majambazi wale walikimbia, baada ya kunyanyuka tuliamua kuanza kukaguana kwanza, tuliona dereva alikuwa amejeruhiwa mkononi na kuna mahabusu wa kike naye alijeruhiwa kichwani lakini hakuna risasi iliyopenya mwilini.
“Wakati tukiendelea kukaguana mahabusu mmoja akaniuliza iwapo kifuani mwangu nimechomwa na kitu, nilipoangalia ndipo nikagundua kwamba kuna kitu kimeingia ndani na baadaye nikajua ni risasi, na hapo ndipo nikaanza kuhisi maumivu,” anasema Sanga aliyejiunga na jeshi hilo mwaka 2000.
Anasema ghafla akaanza kukohoa damu na hapo ndipo walipoamua kumwahisha katika Hospitali ya TMJ ili kupatiwa huduma ya kwanza, kabla ya kumwamishia Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Alisema dhumuni la majambazi hao wanne lilikuwa ni kupora fedha kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa ametokea ATM kuchukua kiasi cha Sh1 milioni.