Mtandao wa Wikipidia umekataa kufuta picha
ambayo Nyani ilijipiga ikisema kuwa kwa sababu
picha hiyo ilipigwa na Nyani ambaye ni mnyama
wala sio binadamu, basi inakuwa mali ya umma.
Hii ni baada ya mpiga picha, mmiliki wa kamera
iliyotumika na Nyani huyo kujipiga picha, kusihi
Wikipedia kufuta picha hiyo na kudai kuwa
Wikipedia ilikuwa inaingilia haki zake za umiliki wa
picha hiyo.
Mpiga picha, David Slater, alikuwa akijaribu kunasa
picha za Nyani kwa masaa kadhaa, wakati ambapo
Nyani mmoja alichukua mojawapo ya kamera za
David na kujipiga mamia ya picha.
Picha hiyo aliyojipiga Nyani bila shaka ni ya
kusisimua na imempeleka David kuwa maarufu
ulimwengu mzima.
La kusikitisha ni kuwa hatimaye Slater sasa
amejipata katika mvutano wa kisheria na Wikimedia
kuhusiana na ni nani hasa mmiliki wa picha hiyo.
David, ambaye hutegemea upiga picha kama jinsi
moja ya kujikimu kimaisha, yuko makini
kuhakikisha picha hiyo imeondolewa kwa tovuti ya
Wikipedia mara moja, huku Wikipedia ikidai kuwa
iwapo kuna mmliki wa picha hiyo basi ni Nyani
aliyejipiga picha hiyo.
Mvutano wa kisheria ilirejelewa kuangaziwa
kufuatia uamuzi wa Wikipedia kuchapisha maombi
yote iliyopata kuhusu kufuta au kuhariri habari au
picha au video zozote ilizoweka kwenye tovuti zao.
Mojawapo ya maombi hayo ni David Slater kutaka
picha aliyojipiga Nyani kuondolewa kwenye tovuti
ya Wikipedia mara moja kwani ikiwa kwenye tovuti
hiyo iko wazi kwa umma.