LICHA ya sheria ya kunyonga kupigiwa
kelele na jumuiya za kimataifa, wajumbe
wa kamati namba sita ya Bunge Maalumu
la Katiba wamependekeza iendelee
kutumika nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari
Mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Steven Wassira, alisema hali
hiyo ilijitokeza wakati wa kujadili Sura ya
nne ya Rasimu ya Katiba.
“Wapo baadhi ya wajumbe walitaka adhabu
ya kifo ifutwe, lakini wengi walipendekeza
adhabu hiyo iendelee, ingawa katika miaka
ya hivi karibuni adhabu hiyo imekuwa
ngumu kutekelezeka,” alisema.
Kwa upande wa suala la uraia wa nchi
mbili, alisema wameliacha kiporo
kutokana na kuwepo kwa mvutano
miongoni mwa wajumbe.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati
hiyo iliiacha kiporo sura hiyo na
kuendelea kujadili sura nyingine.
“Kamati yetu hadi sasa imejadili sura ya
pili, ya tatu na ya nne, Sura ya tano
tuliiacha kiporo, hasa katika suala la
uraia pacha,” alisema.
Alisema suala hilo halikufikia mwisho
kutokana na kuwa na mjadala mkubwa
kutokana na wajumbe kugawanyika na
kwamba hata hivyo, suala hilo litapigiwa
kura ili kupatiwa majibu.
“Maeneo mengi katika kamati yetu
tumekubaliana, lakini yapo maeneo
machache ambayo tunatofautiana,”
alisema Wassira.
Alisema pamoja na kujadili sura hizo,
kamati yake bado haijapiga kura kupitisha
ibara za sura hizo ambayo kwa mujibu
wa sheria inahitajika theluthi mbili ya
wajumbe wote wakati wa kupitisha
maamuzi.
Wassira alisisitiza kwamba Bunge la
Katiba litaendelea na vikao vyake kama
kawaida vya kutunga Katiba.
“Bunge hili haliwezi kuvunjwa kwa sababu
watu wachache hawapo, kama ambavyo
mnaona tunaendelea na vikao vyetu kama
kawaida,” alisema.