DIWANI wa Kata ya Sinza kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Dar, Renatus Pamba ‘Mr. Simple’ anadaiwa kumshushia kipigo denti wa Chuo cha Ubaharia cha EMI jijini Dar, Alpha Mohamed (18) mpaka kumsababishia kupoteza fahamu, Risasi Jumamosi limenyetishiwa.
Kwa mujibu wa mjomba wa Alpha, Aboubakar Ramadhan, tukio hilo lilijiri Agosti 29, mwaka huu nyumbani kwa diwani huyo, Sinza-White Inn ambapo chanzo cha kipigo hicho kikidaiwa kuwa ni denti huyo kukutwa akipiga stori na binti wa diwani aliyejulikana kwa jina la Mage.
Naye Alpha mwenyewe akizungumzia tukio hilo kwa wanahabari wetu, alisema siku hiyo usiku alipigiwa simu na Mage ya kumtaka wakutane ili amjuze kilichojiri kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa rafiki yao mmoja (hakutajwa jina) kwa kuwa Mage hakwenda kwenye shughuli hiyo.
Denti huyo aliendelea kuanika mambo kwamba, muda mchache baada ya kukutana na Mage nje ya nyumba yao, alishangaa kumwona kijana mmoja anatokea na kumwambia anaitwa na diwani huyo nyumbani kwake.
“Mwanzoni nilisita wito huo lakini kwa vile sikuona kama nilikosea chochote niliamua kwenda kwa diwani huyo lakini nikashangaa baada ya kuingia tu, geti likafungwa na kuanza kupelekwa mzobemzobe mpaka sebuleni.“Nilimkuta diwani pale sebuleni ambapo alianza kunishambulia kwa kunipiga fimbo za fagio la njiti huku akisema natembea na Mage.
“Alinipiga kuanzia saa 6 usiku hadi saa 9 maeneo ya kichwani, mgongoni na kifuani. Hali ilivyokuwa mbaya sana, alikwenda chumbani kwake, nami nikajikaza na kupiga simu nyumbani, lakini akaja, akazichukua simu zangu na kuzizima huku akisisitiza kwamba atanipiga zaidi,” alisema Alpha.
Mjomba wa Alpha yeye anasema baada ya kupokea simu ya anko wake huyo, hakujua alikuwa katika nyumba gani zaidi ya kumsikia akiomba msaada, hivyo walianza kumtafuta bila mafanikio kwa kuwa simu zake zote zilikuwa hazipo hewani.
“Tulimtafuta sana huku tukimpigia simu mara kwa mara. Ilipofika saa 9 usiku sasa, kuna mtu akatutonya kwamba, Alpha alionekana akiingia kwa diwani huyo.
“Tulikwenda kwa diwani, tukamkuta Alpha hajitambui hata kidogo. Mwili ulikuwa umevimba, hasa sehemu za kichwani huku mguu wake mmoja umeteguka.“Tulimchukua Alpha na kumpeleka Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar ambapo alipewa PF 3 kwa ajili ya kwenda kupata matibabu, tulimpeleka Hospitali ya Palestina (Sinza).
“Pale, madaktari walitwambia Alpha ameathirika zaidi ndani kwa ndani hasa sehemu za kifuani na mgongoni,” alisema mjomba huyo.Naye mama mzazi wa Alpha, Zanura Ramadhan alisema familia imefungua jalada la kesi lenye Kumbukumbu Na. KN/RB/7748/2014 SHAMBULIO na wamefanikiwa kumkamata kijana ambaye alimw ingiza kwa diwani siku ya tukio.
Diwani huyo alipotafutwa kwa njia ya simu na gazeti hili na kusomewa mashitaka yake, alisema na yeye amefungua mashitaka katika Kituo cha Polisi Urafiki-Ubungo akimtuhumu Alpha kutaka kumbaka binti yake.
“Nikwambie tu, yule Alpha alikuwa na binti yangu Mage usiku na alitaka kumbaka hivyo nimefungua mashitaka na amekamatwa,” alisema diwani huyo.Alipoulizwa kuhusu madai ya kumpiga Alpha, alikana na kusema hakumpiga yeye bali msaidizi wake wa nyumbani (yule aliyemtuma akamwite Alpha).