Featured Posts

Monday, September 15, 2014

DUNIA HII INA MAMBO, MAMA AMTOA KAFARA MWANAE HILI AWE TAJIRI, BABA AKASIRIKA NA KUMUUA MKEWE

MY God! Hali huenda ikigeuka, wakati jamii inaamini akina baba ndiyo wenye tabia ya kutokuwa na uchungu kwa watoto, imekuwa tofauti kwa mama huyu!Ni mkazi mmoja wa Kijiji cha Mwanamonga, Kata ya Lilambo, Manispaa ya Songea, Kasiana Komba (60) anadaiwa kuuawa na mumewe, Allan Menas Lwambano (76) kisa kikidaiwa mambo ya kumtoa kafara mtoto.
Bwana Allan Menas Lwambano anayedaiwa kumuua mkewe.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilijiri usiku wa Agosti 25, mwaka huu ambapo maelezo ya mume huyo yanasema ni baada ya marehemu kumtaka akubali kumuua mtoto wao mmoja (jina tunalo) kati ya saba ili walipe madeni kwa imani ya kishirikina na kufanikiwa katika kipato (utajiri).
RPC wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msekela.
ILIVYOKUWA
Ilielezwa kuwa, mwanaume huyo alikataa ombi hilo na mkewe akamwekea mgomo wa kumnyima unyumba hadi pale atakapokubali ombi lake hilo.
MAISHA YA NDOA
Ilidaiwa kuwa, maisha ya wawili hao yakawa ya ‘sitaki nataka’, mume akitaka unyumba mke hataki kwa vile amemkatalia kumtoa mtoto wao kafara wakati yeye mke alishawaambia wenzake (kwenye ushirikina) kuwa, ameamua kumtoa mtoto huyo lakini baba yake hakutaka kufanya hivyo.
SIKU YA TUKIO
“Siku ya tukio usiku, Lwambano alirudi nyumbani na kumkuta mkewe amelala, alianza kumshikashika mwilini kuashiria alimhitaji faragha, ndipo mke huyo alipotoka nje na kuchukuwa mchi wa kutwangia mahindi kwa lengo la kumpiga mumewe.
Kasiana Komba aliyedaiwa kumtoa kafara mtoto wake ili apate utajili.
“Mumewe aliuzuia, akamnyang’anya na kumpiga mkewe kichwani, alianguka palepale na kufariki dunia,” kilisema chanzo.
MUME AHANGAIKA KUUZIKA MWILI
Habari za ndani zinasema kuwa, mume alipobaini ameua aliuchukuwa mwili wa mkewe na kuupeleka nyuma ya nyumba ambako kuna choo na kuuzika huku akipanda migomba juu ili kuzubaisha watu.
WATOTO: “BABA, MAMA YUKO WAPI?”
Agosti 26, mwaka huu, siku moja tu baada ya tukio hilo la kutisha, watoto ambao wanaishi mbali na nyumba hiyo walifika na walipoona hawamuoni mama yao, walimwuliza baba yao: “Baba, mama yuko wapi?”  akawajibu: “Mama yenu ameenda mjini Songea, atarudi.”
WATOTO WAENDA KWA MGANGA
Ikazidi kudaiwa kuwa, Agosti 27, mwaka huu, watoto hao hawakukubaliana na majibu ya baba yao, wakaenda kwa mganga wa kienyeji (jina halikupatikana mara moja) kwa lengo la kupiga ramli ili kujua alipo mama yao.
Waombolezaji wakiwa msibani.
“Mganga baada ya kuangalia ‘king’amuzi’ chake aliwaambia kama wanataka kujua mama yao alipo, warudi wakamchukue baba yao na kumfikisha kwa mganga huyo kwani yeye (baba) ndiye ana siri nzito.
“Watoto hao wakiongozwa na kaka yao mkubwa (Mathias) walimpa baba yao maagizo ya mganga. Ndipo baba huyo naye akawaambia kama wanataka kujua ukweli wa mama yao alipo, waongozane hadi kwa mtendaji wa kijiji akasimulie mbele yake.
MBELE YA MTENDAJI
Septemba 4, mwaka huu, familia hiyo ikiongozwa na baba mtu walifika kwa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanamonga, Said Mango na Mwenyekiti wa Kijiji, Maria Kahimba ambapo katika maelezo yake , mzee huyo alikiri kumuua mkewe kwa kumpiga na mchi kichwani.
NUKUU YA MUME
Mzee huyo ananukuliwa hivi: “Nimemuua mke wangu nikamfukia nyuma ya nyumba yangu kwenye choo (watu wakapigwa butwaa).
Polisi wakiwa eneo la tukio.
“Sababu kubwa ya chanzo cha tukio ni mke wangu nilimkatalia ombi lake la kutaka tumuue mtoto wetu mmoja ili alipe madeni ya uchawi na kufanikiwa kimapato.
“Nilimkatalia, akawa ananinyima unyumba. Siku ya tukio nilimlazimisha kunipa unyumba, akakataa akataka kunipiga na mchi, nikamuwahi yeye na kumpiga, akakata roho.”
NANI ANAYEJUA?
Mwanamke mmoja aliyekataa kutaja jina lake, aliliambia Uwazi kwamba, marehemu aliwahi kumlalamikia kuhusu mumewe kugoma kumtoa mtoto wao mmoja kafara ili waweze kupata  mali. Alisema mumewe haoneshi kutaka mabadiliko.
“Alisema namwambia mume wangu tumtoe mtoto mmoja kafara tupate utajiri lakini alisema sitaki kusikia habari hizo, kwani yeye ameridhika na ufukara,” alisema mwanamke huyo akimkariri marehemu.
POLISI WAFUKUA MWILI, WAKUTA UMEHARIBIKA
Baada ya maelezo ya mzee huyo, vilio vilitawala, hakuna aliyeamini kisha familia kwa kushirikiana na wananchi na jeshi la polisi,
walifika nyumbani kwa mzee huyo akaonyesha sehemu aliyomfukia mkewe, polisi wakaamuru mwili huo ufukuliwe ukakutwa umeharibika vibaya, hasa sehemu ambazo mchi ulipiga.
Baada ya polisi na madaktari kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, waliwaruhusu wanandugu wauzike.
MTUHUMIWA YUKO POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Mihayo Msikela (pichani), amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria.

TUMEAMIA HUKU