Mshtakiwa hakimu Burugu akipelekwa kwenye chumba maalumu cha washitakiwa kusubiri usafiri wa kumpeleka Gerezani |
Na Mwandishi wetu, Tabora
HAKIMU Osca Bulugu ambaye alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu ya kuomba na kupokea rushwa amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja na nusu au kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela.
Adhabu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Shinyanga Massele John Chaba baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili hakimu Chaba alisema kuwa analazimishwa na matakwa ya sheria kutoa adhabu hiyo kwa mshitakiwa aliyetiwa hatiani na kwamba endapo asiporidhika na uamuzi wa mahakama hiyo anaweza kukata rufaa.
Bulugu alifikishwa mahakamani hapo mnamo mwaka 2013 na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini akikabiliwa na mashitaka matatu moja la kuweka mazingira ya kuomba na mengine mawili ya kupokea rushwa.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Mabula Mapalala ulidai kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo kati ya tarehe 15 hadi 22 marchi 2013 akiwa ni hakimu mkazi wa wilaya ya Urambo.
Ilidaiwa kuwa tarehe 15-03-2013 mtuhumiwa akiwa ni hakimu wa mahakama ya wilaya ya Urambo alimshawishi Lucas Raymond Changala ampe shilingi milioni tano ili aweze kumpa dhamana ya mtoto wake aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi wa fedha za benki ya NMB.
Wakili Mapalala alidai katika shitaka la pili kuwa tarehe 18/03/2013 mtuhumiwa alipokea shilingi milioni moja toka kwa Changala kama malipo ya awali ili aweze kumpa dhamana Phillipo Raymond aliyekuwa mtumishi wa benki ya nmb anayetuhumiwa kuiba zaidi ya shilingi milioni mia moja na ishirini.
Katika shitaka la tatu Mwanasheria huyo wa Takukuru alidai kuwa tarehe 21/03/2013 mtuhumiwa huyo alipokea tena shilingi milioni moja ikiwa ni endelezo la malipo aliyoomba aweze kumpa dhamana mtumishi huyo wa nmb kutoka kwa rafiki wa Philipo ambaye ametajwa kama shahidi wa pili anayefahamika kwa jina la Stela Masokola.
Mara baada ya mahakama kumtia hatiani mshitakiwa upande wa mashitaka ulidai kuwa itolewe adhabu kali ili iwe fundisho kwani wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya rushwa hasa vinavyofanywa na watumishi wa umma hususani watu wenye dhamana ya uongozi.
Naye hakimu Bulugu ili asipewe adhabu kubwa kwa vile ni mkosaji wa mara ya kwanza,alijitetea kuwa hana wazazi na anafamilia ya watu zaidi ya kumi wanaomtegemea yeye wakiwemo watoto wake baada ya kufiwa na mkewe na hivyo kuiomba mahakama impe adhabu nafuu ikiwemo kuachiwa kwa masharti adhabu ambayo aliiona ingemfaa kwa wakati huu.
Baada ya utetezi huo hakimu aliyesikiliza shauri hilo alimhukumu kulipa faini ya shilingi laki tano kwa kila kosa ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa na adhabu hiyo ya kifungo itakwenda pamoja kwa maana ya miaka mitatu kwa pamoja.